DKT. MPANGO ATAKA HATUA ZA PAMOJA NA MSHIKAMANO WA MATAIFA KATIKA UWEKEZAJI ENDELEVU WA BAHARI NA ULINZI WA BIOANUWAI
DKT. MPANGO ATAKA HATUA ZA PAMOJA NA MSHIKAMANO WA MATAIFA KATIKA UWEKEZAJI ENDELEVU WA BAHARI NA ULINZI WA BIOANUWAI

Jumanne, Juni 17, 2025, Ufaransa

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mataifa kuhakikisha kunakuwa na hatua za pamoja, mshikamano wa kimataifa, na uwekezaji endelevu ili kuhakikisha uchumi endelevu wa bahari, kupunguza uchafuzi wa mazingira pamoja na kulinda bioanuwai ya baharini.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akihutubia Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari (UNOC3) akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano huo unaofanyika Jijini Nice nchini Ufaransa.

Amesema hapana budi kuwa na hatua za ujasiri zikazoratibiwa kwa ufanisi ili kuhakikisha maendeleo makubwa katika uendelevu wa bahari. Makamu wa Rais ameongeza kwamba ni muhimu kuongeza ufadhili katika kushughulikia changamoto za bahari, kwa kuzingatia zaidi kusaidia nchi za kipato cha chini na nchi zinazoendelea za Visiwa Vidogo, ambazo zinakabiliwa na ufinyu wa bajeti na mizigo ya madeni inayokwamisha kufikia ahadi zilizofanywa za utekelezaji wa Lengo la Maendeleo Endelevu namba 14.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuhakikisha utekelezaji kamili wa Mkataba wa Bahari Kuu (BBNJ), kushughulikia tishio la uchimbaji madini wa bahari kuu usio endelevu pamoja na kuanzishwa kwa vyombo vya kisheria ili kukabiliana na uchafuzi wa plastiki. Pia amesema ni vema kuimarisha sera za kisayansi ili kukuza uhamishaji wa teknolojia, kutumia uwezo wa uvumbuzi, kuunganisha maarifa ya jadi na asilia na matumizi ya taarifa za wakati halisi ili kuwa na usimamizi bora wa bahari.

Aidha, Makamu wa Rais amesema ni lazima kuwa na ushirikiano jumuishi na wenye usawa unaowezesha jamii za watu wa pwani kuwa wahusika wakuu katika jukumu la kulinda na kuvumbua masuluhisho mbalimbali ya uendelevu wa bahari.

Mkutano huo unawakutanisha Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Kimataifa, Asasi za Kiraia pamoja na Sekta binafsi kwa lengo la kuhamasisha utekelezaji wa Lengo la Maendeleo Endelevu namba 14 (SDG 14) linalolenga kuhifadhi na kutumia  kwa uendelevu rasilimali za bahari, bahari kuu na mazingira ya owani.