MKUU WA WILAYA YA MTWARA AZINDUA RASMI TAMASHA LA MSIMU WA NYANGUMI 2025

Jumatatu, Septemba 22, 2025, Mtwara.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdallah Mwaipaya amewahimiza wananchi na wageni kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo katika Mkoa wa Mtwara, ikiwemo eneo la Msimbati ambko Nyangumi huonekana kwa wingi kuanzia Agosti hadi Novemba kila mwaka.
Mhe. Mwaipaya alitoa rai hiyo tarehe 17 Septemba 2025, wakati akizindua rasmi Tamasha la Msimu wa Nyangumi katika viwanja vya Mashujaa Park.
Akizungumza katika uzinduzi huo, alisema kuwa tamasha la mwaka huu ni fursa kubwa ya kuutangaza Mkoa wa Mtwara kupitia utalii wa bahari, vivutio vya asili na urithi wa utamaduni.
“Pamoja na mambo mengine, kupitia tamasha hili tutashuhudia michezo mbalimbali ikiwemo kuogelea, kuendesha mitumbwi na riadha. Michezo hiyo itafanyika katika fukwe za bahari za Mnazi Bay, hivyo nawahimiza wananchi kushiriki kwa wingi. Nimejulishwa kuwa utaratibu umewekwa vizuri – zitakuwepo boti kwa ajili ya kutembelea visiwa vya Mnazi Bay, kuangalia milima ya mchanga, maingilio ya Mto Ruvuma kwenye Bahari ya Hindi, na kupumzika katika fukwe nzuri za Msimbati,” alisema Mhe. Mwaipaya.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye viwanja vya Mashujaa ili kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika maonyesho hayo ikiwemo Simba na Tausi.
Kwa upande wake, Balozi wa Utalii Mtwara na Mdau wa Uhifadhi, Sameer Murji, akizungumza katika ufunguzi huo, alisema tamasha hilo limebuniwa kwa lengo la kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu uwepo wa nyangumi, kuvutia wageni wa kitalii, na kuwakutanisha wadau wa sekta ya utalii ili kujadili namna ya kukuza utalii hasa wa baharini.
Tamasha la Nyangumi Festival linafanyika kuanzia Septemba 17 hadi 20, 2025, na kilele chake kitafanyika katika fukwe za Msimbati.