MPRU NA WANANCHI WA MAFIA KUSHIRIKI MAFUNZO YA UREJESHWAJI WA MATUMBAWE NCHINI INDONESIA

Jumatatu, Agosti, 2025, Indonesia
Shirika lisilo la kiserikali la Ropes of Hope limewezesha mafunzo ya uhifadhi na urejeshwaji wa matumbawe yaliyofanyika nchini Indonesia kwa muda wa wiki nne kuanzia Agosti 2025. Mafunzo haya yamelenga Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia (MIMP) ambapo watumishi wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) pamoja na wanajamii kutoka Mafia wamepata nafasi ya kushiriki ili kuongeza ujuzi na kuutumia katika kuleta mabadiliko chanya kwenye juhudi za uhifadhi wa matumbawe nchini Tanzania.
Akizungumzia mafunzo hayo, Mhifadhi Bahari wa MPRU, Pascal Mkongola, alisema: “Mafunzo haya ni muhimu kwa taasisi na jamii kwa ujumla katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Kupitia mafunzo haya tunaweza kuimarisha juhudi za urejeshwaji wa matumbawe, ambayo ni rasilimali muhimu kwa ustahimilivu wa mazingira ya baharini na maendeleo ya jamii za pwani.” Washiriki wengine kutoka Jibondo, Mafia ni pamoja na Mikidadi Ahmadi na Hatibu Sheshe, waliowakilisha wanajamii katika safari hii ya kujifunza na kubadilishana uzoefu.
Uhifadhi wa matumbawe una nafasi kubwa kwa jamii za pwani kwani hutoa makazi na mazalia ya samaki na viumbe wengine wa baharini, vinavyotegemewa kama chakula na chanzo cha kipato kupitia uvuvi endelevu. Aidha, miamba ya matumbawe hufanya kazi ya asili ya kulinda fukwe dhidi ya mmomonyoko unaosababishwa na mawimbi makubwa na dhoruba, hivyo kusaidia kulinda makazi ya watu, miundombinu na kuendeleza maisha ya pwani.
MPRU inaendeleza ushirikiano na taasisi ya Ropes of Hope katika elimu na shughuli za urejeshwaji wa matumbawe, sambamba na kuimarisha ushirikiano na taasisi na mashirika mengine ya kitaifa na kimataifa. Ushirikiano huu unalenga kuongeza uelewa, kubadilishana maarifa na teknolojia, pamoja na kujenga uwezo wa pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazotishia ustahimilivu wa mifumo ya ikolojia ya baharini kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.