MPRU YASHIRIKI UZINDUZI WA MRADI WA KUTUNZA MSITU WA MLOLA WILAYA YA MAFIA
MPRU YASHIRIKI UZINDUZI WA MRADI WA KUTUNZA MSITU WA MLOLA WILAYA YA MAFIA

Jumanne, Mei 27, 2025, Mafia

Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) imeshiriki uzinduzi wa mradi wa kutunza msitu wa Mlola utakaoimarisha ustahimilivu wa mifumo ya Ikolojia ya misitu katika Kisiwa cha Mafia, uliofanyika tarehe 26 Mei, 2025.

Mradi huo uliozinduliwa na Shirika linalojihusisha na Uhifadhi wa Mazingira na Viumbe walio hatarini kutoweka Duniani (Sea Sense) unalenga katika  kupambana na kudhibiti changamoto ya Mabadiliko ya Tabianchi ili yasilete madhara katika Msitu wa Mlola uliopo katika Kisiwa cha Mafia.

Akizindua mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Katibu Tarafa wa Kata ya Kusini Ndg. Taifa Constantine amelishukuru Shirika la Sea Sense kwa kushirikiana na Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia (MIMP), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), pamoja na Halmashauri kwa jitihada za kuanzisha mradi huo utakaosaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

"Tumeshuhudia jinsi rasilimali zinavyomalizwa sehemu mbalimbali na zinavyoathirika na mabadiliko ya tabianchi, hivyo tunavyopata wadau kama hawa wanaokuja kurekebisha yaliyotokea, hatuna budi kuwapa ushirikiano ili kufanikisha adhma hiyo" ameeleza Ndg. Constantine.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Sea Sense, Ndg. Gosbert Katunzi ameeleza kuwa mradi huo ukitekelezwa vizuri na kuweka bayana changamoto na fursa zilizopo, utavutia wadau wengi ili waweze kuwekeza kisiwani Mafia.

Wadau mbalimbali wa mazingira wametoa wito kwa mashirika mengine kuunga mkono jitihada mbalimbali za utoaji wa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira ili kuokoa rasilimali zilizopo.

"Tunashukuru shirika la Sea Sense kwa hatua mbalimbali wanazochukua kutunza mazingira, niwaombe mashirika mengine na wadau mbalimbali waunge mkono kutoa elimu kuhusu mazingira maana yanamgusa kila mtu na faida zake kila mtu anazijua, bila mazingira kila kitu kitatoweka" ameeleza Bw. Omari Abdallah, mkazi wa Mafia anayefanya kazi na Shirika la Sea Sense katika Uhifadhi wa Kasa.

Mradi wa kutunza msitu wa Mlola unatarajiwa kutekelezwa kwa miezi 18 katika Vijiji vitatu vya Kungwi, Kibada na Kifinge ambapo utaongeza ustahimilivu kwa jamii katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.