TUSIHUJUMU MAKAZI YA VIUMBE WA BAHARINI KWA UVUVI HARAMU NA TAKA NGUMU- DC MTWARA

Jumamosi, Septemba 20, 2025, Mtwara
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdallah Mwaipaya ameeleza kuwa Tamasha la Nyangumi ni alama ya mshikamano kati ya Uhifadhi wa mazingira, maendeleo ya kiuchumi na urithi wa kitamaduni kwani Nyangumi si tu kivutio cha utalii, bali ni ishara ya maisha ya baharini na urithi wa kizazi cha sasa na kijacho.
Mhe. Mwaipaya alitoa kauli hiyo tarehe 20 Septemba 2025 akihitimisha Tamasha la Nyangumi lililofanyika fukwe za Msimbati.
“Tumeshuhudia wageni kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania na nje ya nchi wakifika hapa Msimbati, Wajariamali wakishiriki katika maonesho ya sanaa, utamaduni na bidhaa. Hii inatupa fundisho kuwa uhifadhi na maendeleo haviwezi kutenganishwa. Tukiulinda urithi huu wa baharini, tunafungua milango ya ajira, mapato na maendeleo endelevu.” Alieleza Mhe. Mwaipaya.
Nyangumi huonekana Mtwara hasa katika Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma-Msimbati (MBREMP), kuanzia mwezi Agosti mpaka Novemba kila mwaka.