MIMP WAENDESHA MAFUNZO YA KLABU ZA MAZINGIRA MASHULENI
MIMP WAENDESHA MAFUNZO YA KLABU ZA MAZINGIRA MASHULENI

Tuesday, 21 May 2024, Mafia

Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia (MIMP) imeendesha mafunzo kuhusiana na  shughuli za uhifadhi ikiwa ni programu maalum kwa ajili ya kutoa mafunzo ya mazingira katika shule za msingi, sekondari hadi vyuo vya kati  kwa ajili ya kuanzisha Klabu za mazingira na kuzijengea uwezo. 

Mafunzo hayo yametolewa kwa jumla ya shule 20 zikiwemo za Msingi (16), Sekondari (4) na chuo kimoja cha VETA ambapo hule hizo zipo ndani ya maeneo ya MIMP ambapo kwa ujumla imelenga kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo jumla ya wanafunzi 840 ambapo wanafunzi 640 ni kutoka shule za msingi, wanafunzi 160 kwa upande wa sekondari na wanafunzi 40 na kutoka chuo cha kati (VETA).

Kupitia mafunzo hayo yaliyotolewa na wataalam kutoka MIMP, wanafunzi walipata kujifunza na kuelewa umuhimu wa bahari na rasilimali zake kama vile mikoko, matumbawe na nyasi bahari pamoja na viumbe vinavyopatikana baharini ikiwemo samaki. Aidha, walipata kufahamu kuhusu Ikolojia na kuweza kuelekezwa njia bora ya uvunaji wa rasilimali za bahari ili kuondokana na hatari inayoweza kuchangia uharibifu wa rasilimali za bahari iwapo kutakuwa na matumizi ya mabomu, nyavu zenye matundu madogo pamoja na mchinji.