Historia ya Hifadhi Bahari

Hifadhi za Bahari ni maeneo maalumu ya baharí, mito, mabwawa ya asili na ziwa yaliyotengwa kisheria ili kuweka usimamizi imara kwa ajili ya kulinda, kuhifadhi na kurejesha bioanuwai, mifumo ikolojia kwa matumizi endelevu ya rasilimali za baharí na uvuvi kama vile samaki, matumbawe, mikoko na nyasi baharí(mwani).

Uhifadhi wa maeneo ya bahari ulianza tangu miaka ya 1970 kupitia Sheria ya Uvuvi Na. 6 ya mwaka 1970 na usimamizi wake ulikuwa chini ya Idara ya Uvuvi. Mnamo mwaka 1994 Serikali kupitia Bunge ilitunga Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Na. 29 ya mwaka 1994 (marejeo 2009 sura 146) ambayo ilianzisha Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kwa ajili ya kuanzisha, kusimamia, kufuatilia na kuendeleza hifadhi za bahari.

Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kwa sasa kinasimamia maeneo 18 ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kwenye Bahari ya Hindi yenye ukubwa wa takriban kilomita za mraba 2,000. Kati ya maeneo hayo, Hifadhi za Bahari ni tatu (3) ambazo ni Kisiwa cha Mafia (Pwani), Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma (Mtwara) na Silikanti (Tanga). Maeneo Tengefu ni 15 ambayo ni visiwa vya Bongoyo, Sinda, Makatube, Pangavini, Funguyasini, Mbudya na Kendwa (Dar es Salaam), Maziwe, Kirui, Ulenge, Kwale na Mwewe (Tanga) na Nyororo, Shungimbili na Mbarakuni (Pwani). Maeneo ya Hifadhi hutengwa kwa kuzingatia uwepo wa bioanuai na mifumo ikolojia adimu (critical habitats), pamoja na kutekeleza malengo endelevu ya kimataifa ya uhifadhi (SDG 14/2030).

  Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kinatekeleza majukumu yake kupitia Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Sura ya 146 ya mwaka 1994 (marejeo ya mwaka 2009).