BI MEENA: MAFIA NI KITUO CHA MAZALIA YA SAMAKI DUNIANI
BI MEENA: MAFIA NI KITUO CHA MAZALIA YA SAMAKI DUNIANI

Tarehe Iliyochapishwa: Ijumaa, Septemba 29, 2023

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena amesema kwamba Mafia ni sehemu nzuri na yenye mazalia mengi ya samaki duniani, na kwamba serikali inaitazama kipikee katika kutekeleza dhana ya uchumi wa buluu.

Bi. Meena ameyasema hayo leo tarehe 29 Septemba wakati wa Kongamano la Uwekezaji katika Uchumi wa Buluu lililofanyika wilayani Mafia katika viwanja vya Mafia Lodge, Utende.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhe. Zephania Sumaye amesema kwamba Wilaya ya Mafia ni eneo zuri kwa uwekezaji katika Uchumi wa Buluu na wilaya imejipanga kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji.

Uchumi wa Buluu umebeba uvuvi, utalii, usafirishaji, pamoja na uhifadhi na ni eneo ambalo ni muhimu kwa kipato cha Taifa pamoja na kuinua uchumi wa wananchi.

 "Kwa Mafia, eneo ambalo tunaweza kuwekeza kwa haraka kwa sasa, ni katika namna ya kufika Mafia. Kwa upande wa usafiri wa maji na anga" Kauli ya Mkurugenzi, Bodi ya Utalli Tanzania (TTB) Damas Mfugale, wakati wa Kongamano la Uwekezaji katika Uchumi wa Buluu, ikiwa ni siku ya pili ya Tamasha la Utalii, Biashara na Uwekezaji, " Mafia Island Festival "