MATUMBAWE NI CHANZO KIKUU CHA MAKAZI YA SAMAKI-KANALI KOLOMBO
MATUMBAWE NI CHANZO KIKUU CHA MAKAZI YA SAMAKI-KANALI KOLOMBO

Alhamisi, 29 Februari 2024, Pwani

Mkuu  wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo amesema, Matumbawe, nyasi bahari na mikoko ni vitu ambavyo havitengamishwi kutokana na umuhimu wake mkubwa katika Bahari kwani faida kubwa ya matumbawe ni kuwa chanzo kikuu cha makazi na mazalia ya samaki, hivyo amewataka wananchi na wavuvi kuhakikisha wanayatunza.

Mkuu wa Wilaya huyo aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa warsha ya Uhifadhi wa Matumbawe (mazalia ya samaki) Baharini katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo iliyopo Wilayani Kilwa, Mkoa wa Pwani.

"Niwasihi tu baada ya warsha hii twendeni tukaimarishe Kamati za mazingira za Vijiji vyetu ili tuweze kuhifadhi matumbawe yetu. Matumbawe ni chanzo na hifadhi ya chakula na mazalia kwa samaki na hupelekea kuwa uvunaji wa samaki wengi na ambao huongezea Halmashauri mapato" Alisema Kolombo.

Aidha, amewaagiza wavuvi kujiunga katika vikundi vidogodogo katika maeneo yao ili waweze kupewa mikopo na boti za uvuvi halali na kuachana na vitendo vya uvuvi haramu unaosababisha hasara ya kupoteza rasilimali za bahari.

                                                                                                          

Naye, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU), Bw. Godfrey Ngupula awali alipokuwa akitambulisha mradi huo, amesema kilichowavutia kufika Wilayani Kibiti na kutaka kuimarisha Uhifadhi wa Matumbawe ni uwepo wa fukwe yenye miamba muhimu inayostahimili mabadiliko ya hali ya hewa.

"Katika km 75.5 za fukwe za kibiti miongoni mwao km 33.3 ni miamba ambayo ni Matumbawe, tunahitaji sana kuhifadhi rasilimali hii muhimu kwakuwa ni adimu sana duniani" Alisema Ngupula.

Aidha, amesema lengo kubwa la kufanya warsha hiyo ni kutaka kujua changamoto zilizopo kwenye maeneo inapopatikana miamba hiyo na kuona nini kifanyike baada ya kuzungumza na wananchi.

Mbali na hayo amewataka wananchi na Wavuvi kwa ujumla kuacha tabia ya uvuvi haramu kwani  uvuvi huo husababisha kuuwa samaki na mazalia yake kwa ujumla ikiwemo Matumbawe.