DC MAFIA ATOA WITO KWA MASHIRIKA BINAFSI KUJIKITA KATIKA UTUNZWAJI WA MAZINGIRA IKIWEMO RASILIMALI ZA BAHARI
DC MAFIA ATOA WITO KWA MASHIRIKA BINAFSI KUJIKITA KATIKA UTUNZWAJI WA MAZINGIRA IKIWEMO RASILIMALI ZA BAHARI

Jumanne, 9 Julai 2024, Mafia

Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo ametoa wito kwa jamii na mashirika binafsi kujikita katika utunzaji wa mazingira ikiwemo rasilimali za bahari hususani utunzaji wa matumbawe. 

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza wakati wa mkutano wa mradi wa 'Coral Reefs Rescue Initiative' (CRRI) uliohusisha wananchi na ngazi mbalimbali za Serikali Wilayani Mafia ambapo amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele sekta ya mazingira nchini. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Uhifadhi wa kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) na Mratibu wa Mradi wa CRRI Bw. Godfrey Ngupula ametoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano mzuri ili kuweza kufikia lengo la mradi. 

"Kuanzia viongozi wa juu, wataalam, wanasheria, Halmashauri, wafanyabiashara na wananchi wote kwa pamoja tuweze kuzungumzia hali ya matumbawe na kuhakikisha tunayahifadhi kwa kuzingatia ripoti zetu mpango mkakati wa kitaifa tulionao tunaenda kuona nini kifanyike kama jamii ili tuhakikishe rasilimali zinatufaa" alisema Ndugu Ngupula.

Wavuvi, wachakataji samaki  pamoja na wakulima wa mwani wamepongeza kuwepo kwa mradi huo wilayani na kuweka nia ya kushirikiana na Serikali katika kutunza mazingira, hasa matumbawe ili kuendelea kunufaika na rasilimali za baharini. 

"Tunaishukuru Serikali kwa kuwa mstari wa mbele kuhifadhi mazingira na kutuwezesha wavuvi na wakulima wa mwani kufanya shughuli zetu, elimu hii itatusaidia kufanya kazi zetu kwa ufanisi mkubwa" alisema Bw. Issa Kombo, Mvuvi na Mchakataji wa samaki.