DKT. EMMANUEL ANDREW SWEKE AANZA RASMI MAJUKUMU MPRU
Jumatano, Februari 25, 2026 Dar es Salaam

Dkt. Emmanuel Andrew Sweke amepokelewa rasmi katika Makao Makuu ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu- MPRU yaliyopo Dar es Salaam tarehe 25/02/2026, kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Meneja wa taasisi hiyo. Mapokezi hayo yalihudhuriwa na Menejimenti ya MPRU pamoja na watumishi wa Makao Makuu (HQ), yakilenga kumkaribisha kiongozi huyo na kuanza ukurasa mpya wa uongozi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Sweke ametoa shukrani kwa Serikali kwa imani waliyoionesha kwake, pamoja na kuwashukuru watumishi wa MPRU kwa mapokezi mazuri. Amesisitiza kuwa mafanikio ya taasisi yanategemea mshikamano, uwajibikaji na kufanya kazi kwa pamoja kama timu moja.
Ameeleza kuwa kwa kutumia ujuzi na ubunifu uliopo miongoni mwa watumishi, taasisi inaweza kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuzigeuza kuwa fursa za maendeleo ya MPRU na taifa kwa ujumla, hususan katika eneo la uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
Aidha, Dkt. Sweke amempongeza Davis Mpotwa, Meneja aliyekuwa akikaimu, kwa uongozi na weledi aliouonesha katika kipindi cha mpito, hatua iliyowezesha utekelezaji wa majukumu ya MPRU bila kuyumba.

