NDEGE NYUKI KUHIFADHI RASILIMALI BAHARI
NDEGE NYUKI KUHIFADHI RASILIMALI BAHARI

Tarehe Iliyochapishwa: Jumanne, Disemba 05, 2023

Siku tano za mafunzo na uthibitishaji (training and certification) wa Uongozaji wa Ndege nyuki (Advanced Ndege nyuki Piloting) kwa Wahifadhi Bahari wawili wa Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania zimekamilika.

Mafunzo haya yamekuwa ni muendelezo wa mafunzo yaliyoendeshwa kwa takribani miezi (5) ambayo yamekuwa yakifanyika kwa awamu kupitia nadharia na kazi za uwandani.

Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo washiriki katika ujuzi wa kurusha Ndege nyuki kwa Usalama, Sheria zinazosimamia matumizi ya anga, aina mbalimbali za Ndege nyuki na matumizi yake,masuala muhimu ya kuzingatia na majukumu ya Muongozaji Ndege nyuki pamoja na mazoezi kwa vitendo, sambamba na utumiaji wa Ndege nyuki katika uchoraji wa ramani (mapping) na Remote sensing.

Mafunzo haya yalihitimishwa kwa mitihani ambayo inahusika na sifa za kutunukiwa vyeti pamoja na leseni. Mafunzo yalitolewa na Tanzania Flying Labs kwa ufadhili wa Mradi wa Blue Action Fund (BAF) ambao unasimamiwa na WWF-Tanzania kuanzia tarehe 6 hadi 10 Novemba 2023 kwenye ukumbi wa Amverton Tower ulioko Masaki Dar es Salaam.

Baada ya mafunzo haya Mhifadhi Bernard Ngatunga alikiri kupata utaalamu ambao utamsaidia katika kutekeleza majukumu yake kwa urahisi zaidi.

Akizungumzia zaidi upande wa uhifadhi rasilimali Bahari hususani katika kufanya Doria, badala ya kutumia boti kila siku, sasa itatumika Ndege nyuki ambayo itarushwa na kuzunguka maeneo mbalimbali ili kufanya ukaguzi.

Taarifa za Ndege nyuki zitatumika kufanya maamuzi ya eneo gani linaonesha kuwa na uharibifu zaidi kabla ya kupeleka Boti kwa ajili ya Kwenda kudhibiti watu wafanyao uharibifu.

Kwa upande wake Mshiriki mwingine, Mhifadhi Masanja Joram alieleza namna ambayo Ndege nyuki zitasaidia kwenye kurahisisha shughuli za uhifadhi ikiwa ni Pamoja na kufanya tathmini ya ukubwa na hali halisi ya rasilimali mbalimbali za bahari hususani Misitu ya Pwani na Misitu ya Mikoko.Ndege nyuki zitaweza kurushwa hata kwenye maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi.

Zitasaidia kupunguza gharama za usimamizi hasa matumizi ya mafuta ya boti, itasaidia kupunguza matukio ya hatari kama kuzama au kuumia ambayo yangeweza kutokea, halikadhalika Ndege nyuki zitaweza kutumika kwenye utafutaji na uokoaji.

Wahifadhi wawili wamehitimu na kupata leseni za kutumia ndege nyuki za aina mbili, ambazo ni Rotary wings (quadcopter) na Fixed wings kwenye shughuli zao za Uhifadhi.