WAZIRI KAIRUKI AKABIDHI CHETI CHA USHIRIKI SITE 2023
WAZIRI KAIRUKI AKABIDHI CHETI CHA USHIRIKI SITE 2023

Tarehe Iliyochapishwa: Jumapili, Octoba 08, 2023

Waziri wa Maliasili na Utalii Bi. Angellah Kairuki amekabidhi cheti cha ushiriki kwa  Hifadhi  za Bahari na Maeneo Tengefu nchini katika siku ya kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Utalii nchini  (SITE 2023) yaliyodumu kuanzia Agosti 6-8 katika eneo la Mlimani City, Dar es Salaam.

Mhe. Kairuki amekabidhi cheti hicho leo Agosti 8, 2023 na kupokelewa na Afisa Utalii wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu nchini Bw. Davis Mpotwa.

Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu walipata fursa ya kushiriki katika Maonesho hayo ya Kimataifa ya Utalii nchini ambapo ilipata nafasi ya kujitangaza kwa watalii waliofika katika banda kuhusu maeneo yake ya utalii kama vile Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia (MIMP), Hifadhi ya Bahari ya Tanga Silikanti (TACMP), Mfumo wa Hifadhi ya Bahari ya Dar es Salaam (DMRS) na Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingiliano ya Mto Ruvuma (MBREMP) pamoja na shughuli nzima za uhifadhi zinazofanywa nchini kupitia taasisi hiyo.

Katika kuhitimisha Maonesho hayo ya SITE 2023, Mhe. Kairuki amewataka waandaji kuanza maandalizi mapema zaidi ya SITE 2024 kuwa makubwa na bora zaidi ya haya na kuwaomba wagenii kuwekeza nchini Tanzania.

“Napenda kuitaka timu yangu ianze kujiandaa na SITE 2024 tuanze kuiandaa sasa ili kufanya makubwa ili tujivunie lakini pia tuhakikishe waonyeshaji wote na wanunuzi na washiriki wote wanafanikiwa na mtandao na kuendelea kufanya maendeleo zaidi katika biashara zao lakini pia katika utangazaji wa utalii" alisema Mhe. Kairuki.

Tafadhali endeleeni kuja kuwekeza pia Tanzania tunawakaribisha kufanya biashara Tanzania na kuwekeza kama tulivyowasilisha jana kuwa tuna biashara na mazingira mazuri ya uwekezaji pia” aliongezea Mhe. Kairuki

Aidha, Mhe. Kairuki katika kuhitimisha amewashukuru sana watanzania kwa uthubutu wao kwa  kuhudhuria na kujitokeza kwa wingi katika Maonesho ya SITE 2023 kujionea yaliyosheheni katika sekta ya utalii nchini.