MBREMP YAHAMASISHA WANAFUNZI KUHUSU UTALII NA UHIFADHI WA BAHARI MTWARA
MBREMP YAHAMASISHA WANAFUNZI KUHUSU UTALII NA UHIFADHI WA BAHARI MTWARA

Jumatano, Aprili 29, 2026, Mtwara

Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingiliane ya Mto Ruvuma (MBREMP) imefanya ziara ya uhamasishaji katika baadhi ya shule za msingi na sekondari mkoani Mtwara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza utalii wa ndani na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa rasilimali za bahari.

Ziara hiyo imefanyika leo tarehe 29 Aprili, 2026 ikiongozwa na Afisa Utalii, Bi. Rosemary Tadey Kavishe, kwa kushirikiana na Mhifadhi Bahari, Bw. Mustapha Issa Ng’ombo ambapo waliwasilisha mada mbalimbali zilizolenga kuelezea umuhimu wa utalii wa bahari, fursa zilizopo katika sekta hiyo, pamoja na mchango wake katika kukuza uchumi na kuhifadhi mazingira.

Shule zilizofikiwa katika ziara hiyo ni Medi Primary School, Heritage Primary School, King David Primary School, Ruvula Primary School, pamoja na Aquinas Secondary School. Katika kila shule, timu ya wataalamu ilikutana na uongozi wa shule na kufanya majadiliano kuhusu mbinu bora za kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Aidha, walimu na viongozi wa shule hizo walipata nafasi ya kuuliza maswali na kujadili kwa kina namna ya kuwahamasisha wanafunzi kushiriki katika shughuli za utalii na uhifadhi wa mazingira ya bahari. 

Halikadhalika, kupitia mazungumzo na walimu pamoja na viongozi walionesha mwitikio chanya kutoka kwa shule husika, ambapo baadhi yao walitoa mwaliko kwa wataalamu wa MBREMP kurejea tena kwa ajili ya kutoa elimu zaidi ya uhifadhi wa bahari kwa wanafunzi.

Hatua hiyo inatarajiwa kusaidia kuongeza uelewa mpana kwa wanafunzi kuhusu umuhimu wa kulinda bahari na viumbe wake, sambamba na kukuza ari ya kushiriki katika utalii wa ndani.