MENEJA MPRU AANZA ZIARA YA KIKAZI KATIKA VITUO VYA TMRS NA TACMP TANGA
MENEJA MPRU AANZA ZIARA YA KIKAZI KATIKA VITUO VYA TMRS NA TACMP TANGA

Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Dkt. Emmanuel Sweke, ameanza ziara ya kikazi ya siku mbili katika vituo vya Tanga Marine Reserve System (TMRS) na Tanga Coelacath Marine Park (TACMP) mkoani Tanga Machi 18, 2026.

Katika siku ya kwanza ya ziara hiyo, Dkt. Sweke ametembelea wadau mbalimbali wanaoshirikiana kwa karibu na MPRU, wakiwemo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kupitia Kikosi cha Polisi Wanamaji (Marine Police) pamoja na Jeshi la Wanamaji (Navy), kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa rasilimali za bahari.

Akizungumza katika mikutano hiyo, Dkt. Sweke amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano baina ya taasisi hizo ili kuhakikisha juhudi za uhifadhi zinaimarika sambamba na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, hatua itakayochangia kukuza uchumi wa buluu.

Aidha, Dkt. Sweke ametembelea maeneo mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo fungu la mchanga la Nyuli, Kisiwa cha Toten kinachojulikana pia kama “Island of the Dead”, pamoja na visiwa vya Mwewe na Kilui. Lengo la ziara katika maeneo hayo lilikuwa ni kujionea shughuli za utalii zinazoendelea, kutathmini fursa zilizopo, pamoja na kuandaa mikakati ya kuongeza thamani ya maeneo hayo na kuimarisha mazao ya utalii wa baharini.

Ziara hiyo inatarajiwa kuendelea kesho, ambapo Dkt. Sweke atazungumza na watumishi pamoja na wanajamii wanaozunguka maeneo ya hifadhi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano, uwajibikaji na usimamizi shirikishi wa rasilimali za bahari.