MENEJA MPRU AFUNGA MAFUNZO YA MASUALA YA UWEKEZAJI NA UBIA (PPP)
MENEJA MPRU AFUNGA MAFUNZO YA MASUALA YA UWEKEZAJI NA UBIA (PPP)

13 Machi, 2026                Kibaha, Pwani

Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Dkt. Emmanuel A. Sweke, amefunga mafunzo yaliyolenga kuimarisha uwezo wa kiutendaji kwa Menejimenti ya MPRU katika kusimamia masuala ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) pamoja na uwekezaji ndani ya Maeneo ya Hifadhi za Bahari.

Mafunzo hayo yalijumuisha mada mbalimbali ikiwemo uelewa wa dhana ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), mawasiliano na ushawishi katika masuala ya uwekezaji, usimamizi wa mikataba pamoja na mifumo ya biashara katika utalii wa baharini.

 

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Dkt. Sweke alisema kuwa mafunzo hayo ni chachu muhimu katika kuimarisha uwekezaji wa miradi mikubwa ya baharini inayolenga kukuza na kuinua uchumi wa buluu nchini. Alisisitiza kuwa uwekezaji katika rasilimali za bahari unaweza kuleta tija zaidi pale unapotekelezwa kwa kushirikisha sekta binafsi kwa kuzingatia kanuni na miongozo iliyowekwa.

Mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 13 Machi 2026 katika Ukumbi wa TNMC, Kibaha mkoani Pwani, yaliwezeshwa na mtaalamu kutoka Kituo cha Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPPC), Dkt. Bravius Kayhoza, ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya uwekezaji na mawasiliano ya umma.

 

Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Undelezaji wa Rasilimali za Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji (TASFAM) unaotekelezwa na taasisi ya MPRU, ambao umewezesha kufanyika kwa mafunzo hayo kwa lengo la kuimarisha uwezo wa taasisi katika kusimamia uwekezaji na ubia ndani ya maeneo ya hifadhi za bahari.

Aidha, Dkt. Sweke aliipongeza Menejimenti ya MPRU kwa kushiriki mafunzo hayo na kuwataka kuendelea kujifunza na kutumia maarifa waliyoyapata ili kuimarisha usimamizi wa uwekezaji katika maeneo ya hifadhi za bahari.