MENEJA MPRU AHIMIZA USHIRIKIANO, UADILIFU NA UBUNIFU KWA WATUMISHI TANGA

Alhamisi Machi 19, 2026, Tanga
Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Dkt. Emmanuel Sweke, amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili katika vituo vya Tanga Marine Reserve System (TMRS) na Tanga Silikanti (TACMP) mkoani Tanga leo Machi 19, 2026, kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano, uadilifu na ubunifu kwa watumishi.
Katika siku ya pili ya ziara hiyo, Dkt. Sweke alipata fursa ya kufanya kikao na watumishi wa MPRU Tanga, ambapo alijitambulisha na kusikiliza maoni pamoja na changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Sweke amepongeza vituo vya TMRS na TACMP kwa kupokea watumishi wapya sita, hatua ambayo itachangia kuimarisha nguvu kazi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za bahari.
Aidha, amewataka watumishi kuendeleza ushirikiano, kufanya kazi kwa ubunifu, na kuongeza tija katika rasilimali na mazao ya utalii wa baharini ili kuongeza mapato na kuchangia maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla. Pia amesisitiza umuhimu wa uadilifu katika utendaji kazi, akibainisha kuwa kila mtumishi ana wajibu wa kulinda na kuendeleza rasilimali za bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Awali, katika mwendelezo wa ziara hiyo, Dkt. Sweke alitembelea Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bi. Ester Gama, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji. Vilevile, alikutana na uongozi wa Kijiji cha Ushongo ambapo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya MPRU na jamii katika juhudi za uhifadhi na kukuza utalii wa baharini.
Ziara hiyo imehitimishwa ikiwa ni sehemu ya jitihada za MPRU kuimarisha usimamizi shirikishi wa rasilimali za bahari, kwa kushirikiana na wadau na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.

