MIMP YASHIRIKI KATIKA UZINDUZI WA JUKWAA LA VIJANA, YATANGAZA FURSA YA UTALII KATIKA KISIWA CHA MAFIA
MIMP YASHIRIKI KATIKA UZINDUZI WA JUKWAA LA VIJANA, YATANGAZA FURSA YA UTALII KATIKA KISIWA CHA MAFIA

Jumatatu, Aprili 20, 2026, Mafia

Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia (MIMP) ilishiriki katika Uzinduzi wa Jukwaa la Vijana (Vijana Platform) na kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira ya bahari pamoja na fursa mbalimbali zilizopo ndani ya sekta hiyo ya uhifadhi.

Akizungumza katika kongamano hilo lililofanyika Aprili 20, 2026 katika Shule ya Sekondari Kitomondo iliyopo Wilayani Mafia katika Mkoa wa Kilwa, Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo aliyekuwa Mgeni rasmi aliwasisitiza vijana Wilayani Mafia kuwa wabunifu pamoja na kuwa wepesi katika kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ikiwemo mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, uwezeshaji wa vijana kupitia Jukwaa la Vijana, pamoja naafunzo mbalimbali yatolewayo na Serikali na wadau.

Naye kwa upande wake, Mhifadhi Bahari Bw. Ailars Lema alisisitiza umuhimu wa vijana kuwa wabunifu katika kutatua changamoto za mazingira ya bahari, huku akibainisha kuwa sekta ya utalii wa bahari ni chanzo kikubwa cha ajira na kipato.

“Vijana tusibaki kuwa walalamishi, bali tuangalie changamoto za mazingira kama fursa za ubunifu ili kuleta suluhisho endelevu na maendeleo katika jamii zetu,” alisema Bw. Ailars.

Aidha, alieleza kuwa Kisiwa cha Mafia kina hazina kubwa ya vivutio vya utalii wa bahari vinavyoweza kuwanufaisha vijana kiuchumi iwapo watavitumia ipasavyo kama vile utalii wa kupiga mbizi (diving) na kuogelea na Nyangumi (whale sharks), utalii wa fukwe zenye mandhari ya kuvutia, pamoja na matembezi ya kutazama viumbe mbalimbali wa baharini wakiwemo Kasa na Matumbawe.

Pia alitaja fursa za uwekezaji na ajira katika shughuli za uongozaji watalii (tour guiding), uendeshaji wa boti za watalii, ujasiriamali wa huduma za malazi (eco-lodges), pamoja na biashara za bidhaa za asili na sanaa zinazotokana na rasilimali za bahari.

Uzinduzi wa Jukwaa la Vijana umeonekana kuwa chachu muhimu ya kuwaunganisha vijana, kuwajengea uwezo na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za maendeleo, hususan katika sekta ya uhifadhi wa bahari na utalii endelevu katika Kisiwa cha Mafia.