MPRU MBIONI KUANZISHA HIFADHI MPYA YA BAHARI KILWA
Jumamosi, Julai 04, 2026. Kilwa

Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Dkt. Emmanuel Sweke, amefanya ziara ya siku tatu kuanzia Julai 2 hadi Julai 4, 2026 katika Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi, ikiwa ni sehemu ya hatua za awali za uanzishwaji wa Hifadhi mpya ya Bahari ya Kilwa.
Katika ziara hiyo, Dkt. Sweke alikutana na wadau mbalimbali kwa ajili ya mashauriano na uhamasishaji kuhusu mpango huo, ambapo alifanya mazungumzo na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kilwa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, pamoja na ofisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama (TAWA) Wilaya ya Kilwa, sambamba na viongozi wa Kata ya Songosongo.
Mazungumzo hayo yalilenga kuweka msingi wa uelewa wa pamoja kuhusu uanzishwaji wa hifadhi hiyo mpya, ambayo inalenga kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za bahari pamoja na kukuza fursa za utalii endelevu katika eneo hilo.
Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya MPRU kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Na. 29 ya mwaka 1994, ambayo pamoja na mambo mengine inaipa taasisi hiyo wajibu wa kuanzisha, kuendeleza na kusimamia hifadhi na maeneo tengefu ya bahari ili kulinda mifumo ya ikolojia na bioanuai muhimu kwa uendelevu wa rasilimali za bahari na pwani.

