WATUMISHI WATANO MPRU WATUNUKIWA VYETI MAFUNZO YA 'RESCUE DIVING, EMERGENCY FIRST RESPONSE (EFR)

Ijumaa, Aprili 11 2025, Mafia
Watumishi watano (5) wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) wametunikiwa vyeti katika fani za 'Rescue Diving na Emergency First Response (EFR), kufuatia mafunzo ya wiki mbili yaliyofanyika katika Kisiwa cha Mafia.
Mafunzo hayo yaliwezeshwa na Shirika la Plongeurs Du Monde kutoka Ufaransa (Wapiga Mbizi wa Dunia) yenye dhamira ya MPRU katika kuimarisha uwezo wake wa kiutendaji pamoja na kulinda mazingira ya baharini ya Tanzania yenye thamani kubwa.
Watumishi wa MPRU waliokamilisha mafunzo haya kwa mafanikio ni Daniel Mallya, Hashim Kilawi, na Ailas Lema kutoka Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia (MIMP), Maria Pentzel kutoka Makao Makuu ya MPRU, pamoja na Kabodo kutoka Hifadhi ya Bahari ya Tanga Silikanti (TACMP).
Katika mafanikio ya kihistoria, Masanja Joram alishiriki mafunzo maalum ya kwanza kabisa duniani ya 'Eco-Guide Specialty' yenye ithibati ya PADI ambayo yatamwezesha kukuza utalii rafiki kwa mazingira na kuhakikisha mwingiliano endelevu na mfumo wa bahari.
Mpango huu wa kujenga uwezo ni hatua muhimu katika kuwawezesha watumishi wa MPRU kupata ujuzi wa msingi katika ufuatiliaji wa kina cha maji (underwater monitoring), mwitikio wa dharura (emergency response), na mwongozo wa utalii wa mazingira (eco-tourism guidance).
Mhifadhi Mfawidhi wa MIMP, Bw. Amin Abdallah pamoja na Mhifadhi, Mohamed Shamte walihudhuria hafla ya kutunuku vyeti na kuonesha fahari yao kwa mafanikio ya washiriki na kujitolea kwao katika kujifunza.