MPRU YAELEZA UMUHIMU WA UHIFADHI WA BAHARI KATIKA KUKUZA UCHUMI WA BULUU

Jumatatu Agosti 18, 2025 Dar es Salaam
Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) imeshiriki kikamilifu katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yaliyofanyika kuanzia Agosti 1–8, 2025 jijini Dodoma. Ushiriki huo uliolenga kuelimisha umma na wadau kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali za bahari kwa maendeleo endelevu. Maonesho haya yametoa nafasi kwa MPRU kutangaza shughuli mbalimbali za uhifadhi na ulinzi wa rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kupitia maonesho haya, MPRU imeeleza juhudi zake katika kulinda na kuendeleza rasilimali muhimu ikiwemo matumbawe, nyasi bahari, mikoko, pamoja na ulinzi wa viumbe vya baharini na ikolojia ya bahari kwa ujumla. Aidha, ilisisitiza mchango wa rasilimali hizo katika kukuza uchumi wa buluu na kutoa fursa za ajira na uwekezaji.
Akizungumza katika banda la MPRU, Afisa Masoko wa MPRU, Bi. Halima Tosiri, amebainisha vivutio mbalimbali vya utalii wa baharini vilivyo chini ya usimamizi wa MPRU, ambavyo vinajulikana kwa fukwe za kuvutia, michezo ya majini, na uwepo wa viumbe wakubwa wa baharini kama vile pomboo, papa potwe, nguva (Dugong) na nyangumi.
“Tunaelekea kwenye msimu wa nyangumi katika Hifadhi ya Bahari ya Maingilio ya Mto Ruvuma–Mnazi Bay. Tutakuwa na Tamasha Kubwa la Nyangumi litakalofanyika Mtwara mjini sambamba na safari maalumu za kuwaona nyangumi katika eneo la Mnazi Bay,” amesema Bi. Tosiri.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Bw. Davis Mpotwa, alisema kuwa MPRU inaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa uhifadhi ili kuhakikisha rasilimali za bahari zinalindwa na kunufaisha taifa kwa muda mrefu.
“MPRU inatekeleza mradi wa urejeshwaji wa matumbawe nchini kote. Hivi sasa tupo katika hatua ya kutoa elimu kwa jamii za pwani kuhusu umuhimu wa matumbawe ili kushiriki kikamilifu katika kuyahifadhi na kutunza rasilimali za bahari,” amesema Bw. Mpotwa.
Kwa ujumla, ushiriki wa MPRU katika maonesho ya Nane Nane 2025 umeendelea kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu nafasi ya uhifadhi wa bahari katika kukuza uchumi wa buluu na kuendeleza sekta ya utalii wa baharini nchini.