MPRU Yaendesha Warsha ya Kuhuisha Mpango wa Jumla wa Uhifadhi kwa DMRS
MPRU Yaendesha Warsha ya Kuhuisha Mpango wa Jumla wa Uhifadhi kwa DMRS

 

20 Desemba 2025 — Dar es Salaam

Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) imeongoza warsha ya siku mbili ya kupitia na kuhuisha Mpango wa Jumla wa Uhifadhi (General Management Plan – GMP) wa Dar es Salaam Marine Reserves System (DMRS), warsha inayofanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa.

Warsha hiyo ilifunguliwa rasmi na Kaimu Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Bw. Davis Mpotwa, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuwa na GMP iliyoimarishwa ili kukidhi mahitaji ya sasa ya uhifadhi wa bahari. Akizungumza wakati wa ufunguzi, alibainisha kuwa mabadiliko ya kimazingira, kijamii na kiuchumi yanahitaji mipango inayopimika na inayotekelezeka, hivyo kufanya mchakato wa mapitio kuwa hatua muhimu kwa kituo cha DMRS.

 

Kwa kuzingatia hayo, warsha imewakutanisha wadau kutoka Taasisi za Kiserikali, Sekta Binafsi, Asasi zisizo za Kiserikali (NGOs), pamoja na watafiti na wataalamu wa masuala ya bahari. Kupitia majadiliano yao, wadau wamekuwa wakichambua maeneo muhimu ya GMP kwa lengo la kuoanisha mpango huo na hali halisi ya sasa ya kiikolojia na maendeleo ya jamii za pwani.

 

Katika mazungumzo na wadau mbalimbali akiwemo Magreth Nkya, Mtendaji wa Kata ya Tungi (Kigamboni), amesema kuwa “Mapitio haya yataleta tija kubwa kwa sababu yameshirikisha wadau kuanzia hatua za awali. Wadau wa uhifadhi wa bahari wanafahamu changamoto hizi kwa karibu, hivyo ushirikishwaji huu utafanikisha nyenzo hii (GMP) na kuleta matokeo chanya kwa uchumi na jamii za pwani pamoja na taifa kwa ujumla.”

Akiongeza kuhusu umuhimu wa ushirikiano, Fadhili Makwala, Makamu Mwenyekiti wa BMU, alisema: “Ushirikiano kati ya MPRU na BMU umeendelea kuboresha hali ya uhifadhi kwenye maeneo ya hifadhi. Ni muhimu kuimarisha ulinzi wa rasilimali za bahari kwa kufanya kazi pamoja, hasa katika kutoa elimu ya uhifadhi ili jamii iwe na uelewa mpana wa matumizi endelevu ya rasilimali hizo.”

 

Warsha hii ni sehemu ya jitihada za jitihada endelevu za MPRU kuhakikisha kuwa usimamizi wa maeneo ya Baharini unaendana na mabadiliko ya mazingira, mahitaji ya jamii na dira ya taifa ya uhifadhi wa rasilimali za bahari