MPRU YAFANIKIWA KUWEKA MIPAKA KATIKA ENEO TENGEFU LA SHUNGIMBILI MIMP

Alhamisi, Aprili 10 2025, Mafia
Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) imefanikiwa kukamilisha zoezi la uwekaji wa mipaka ndani ya Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia (MIMP) katika eneo tengefu la Shungimbili ambapo zoezi hilo limefanyika kwa mafanikio makubwa kupitia juhudi za timu ya Wahifadhi Bahari wa MPRU.
Vifaa maalum vimetumika kuonesha mipaka hiyo ikiwa ni pamoja na maboya (buoy), pingu za chuma (shackles), minyororo (chain) na vifaa vya kiunganishi vinavyozunguka (swivels). Uwekaji wa mipaka huu ni hatua muhimu ya kiutawala inayolenga kuimarisha Uhifadhi wa maeneo ya baharini na kuwezesha matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo.
MPRU ina jukumu la kuhakikisha maeneo yake yote yanapimwa na kuwekewa mipaka kwa usahihi ili kusaidia kudhibiti matumizi holela ya rasilimali za Bahari, kuzuia uharibifu wa mazingira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa buluu.
Halikadhalika, hatua hii inalenga kupunguza migogoro kati ya Wahifadhi na watumiaji wa rasilimali za Bahari katika maeneo yanayohifadhiwa (MPAs) ambapo vifaa vilivyotumika kwenye zoezi hili vilinunuliwa kupitia mradi wa Blue Action Fund (BAF) unaotekelezwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) katika Wilaya ya Mafia.
Mradi huu ni sehemu ya mpango mpana wa RUMAKI Seascape unaojumuisha maeneo ya Rufiji, Mafia na Kilwa wenye lengo la kulinda na kusimamia rasilimali za Baharini kwa njia endelevu.
Aidha, MPRU inaendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa katika juhudi za kuhifadhi mazingira ya Baharini pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi endelevu ya rasilimali za Bahari na kuhamasisha njia mbadala na rafiki kwa mazingira za kujipatia kipato kama vile kilimo cha Mwani.