MPRU YAFIKIA WANANCHI KWA WINGI KATIKA MAONESHO YA NANE NANE – LINDI

Jumatatu Agosti 18, 2025 MTWARA
Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) kupitia Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma (MBREMP) imeshiriki kikamilifu katika maonesho ya Nane Nane yaliyofanyika viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi. Ushiriki huo ulilenga kutoa elimu na uhamasishaji kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa bahari na rasilimali zake kwa maendeleo endelevu ya jamii na taifa kwa ujumla.
Katika banda la MPRU, wananchi walipata elimu ya sera, sheria na kanuni za uvuvi, uvuvi endelevu wenye tija kwa jamii na mazingira, umuhimu wa utalii wa baharini na viumbe wake adimu kama vile nyangumi, samaki na viumbe wengine, lishe bora kupitia ulaji wa samaki, dagaa na mazao mengine ya baharini, madhara ya uvuvi usiokubalika pamoja na dhana za uvuvi halali.
Kupitia maonesho haya, zaidi ya watu 1,200 walitembelea banda la MPRU na kujifunza kuhusu fursa na manufaa yanayotokana na uhifadhi wa bahari. Vifaa mbalimbali vya kielimu ikiwemo mabango, flip charts na vielelezo vya viumbe vya baharini vilitumika kufikisha elimu kwa wananchi.
MPRU itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha jamii zinaelimishwa kuhusu umuhimu wa rasilimali za bahari, ili kukuza uchumi wa buluu na kutunza mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.