MPRU YAKUTANISHA WADAU KUJADILI FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA UTALII WA BAHARINI
MPRU YAKUTANISHA WADAU KUJADILI FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA UTALII WA BAHARINI

Jumanne          Machi 24, 2026, Dar es Salaam

Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) imekutana na wadau wa sekta ya utalii wa bahari na fukwe katika warsha maalum iliyofanyika leo, Machi 24, 2026, katika ukumbi wa Peacock Hotel, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji pamoja na kuimarisha ushirikiano katika kukuza uchumi wa buluu.

Warsha hiyo imewaleta pamoja wadau mbalimbali, wakiwemo wataalamu kutoka MPRU, taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na wadau wa utalii, ambapo mada kuu zilizowasilishwa zilihusu fursa za uwekezaji katika Hifadhi za Bahari (MPAs), taratibu za uwekezaji katika maeneo hayo, pamoja na mazingira ya uwekezaji na changamoto zinazokabili uwekezaji katika utalii wa bahari.

 

Kupitia mada hizo, washiriki walipata uelewa wa kina kuhusu mifumo ya uwekezaji, ikiwemo ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), pamoja na mbinu bora za kuendeleza shughuli za utalii wa baharini kwa kuzingatia kanuni za uhifadhi wa rasilimali.

Aidha, mijadala iliyofanyika imewezesha wadau kubadilishana uzoefu na mawazo kuhusu namna bora ya kutumia fursa zilizopo katika hifadhi za bahari, huku wakizingatia matumizi endelevu ya rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

 

Warsha hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa TASFAM unaolenga kuimarisha usimamizi wa hifadhi za bahari pamoja na kukuza uwekezaji na utalii endelevu nchini.