MPRU YASHIRIKI SEMINA YA MAFUNZO YA ‘SATELLITE REMOTE SENSING APPLICATION’ NCHINI CHINA

Jumatano, Aprili 23, 2025, China
Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) imeshiriki semina ya mafunzo ya ushirikiano kati ya China na Afrika kuhusu Matumizi ya Teknolojia ya Satelaiti kwa Ufuatiliaji wa Rasilimali (Satellite Remote Sensing Application), iliyofanyika kwa wiki mbili (2) kuanzia Februari 19-Machi 4 2025 jijini Beijing, China.
Tanzania imewakilishwa na maafisa kutoka MPRU, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Maliasili na Utalii, na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), sambamba na wajumbe kutoka nchi nyingine saba (7) za Afrika pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Afrika.
Mhifadhi Bahari, Bw. Mustapha Issa kutoka Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingiliano ya Mto Ruvuma (MBREMP) ameiwakilisha MPRU. Kupitia semina hiyo amepata ujuzi wa vitendo katika matumizi ya teknolojia ya remote sensing, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa miamba ya Matumbawe, mabadiliko ya fukwe, na kubaini shughuli za uvuvi haramu.
Semina ilijikita katika matumizi ya teknolojia za kisasa za satelaiti, ikiwa ni pamoja na akili bandia (AI) na ujifunzaji wa mashine (machine learning), katika kusaidia ufuatiliaji wa mazingira, Uhifadhi wa bayoanuwai, na Usimamizi wa Rasilimali za Baharini.
Semina hiyo iliandaliwa na Kituo cha Ushirikiano wa China na Afrika kuhusu Matumizi ya Satelaiti (China-Africa Cooperation Center on Satellite Remote Sensing Application - CACSA), kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiufundi na kubadilishana maarifa katika teknolojia ya satelaiti.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuimarisha uwezo wa MPRU katika shughuli za Uhifadhi wa rasilimali za bahari unaoongozwa na takwimu, pamoja na kusaidia maendeleo ya mifumo ya ufuatiliaji kwa muda halisi (real time) kwa ajili ya kuongeza ujuzi wa kiufundi na kuboresha juhudi za Uhifadhi.