MPRU YASHIRIKI UZINDUZI WA MKAKATI WA KITAIFA WA KUSIMAMIA NA KUENDELEZA MISITU YA MIKOKO

Jumatano, Agosti 06, 2025, Dar es Salaam
Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) imeshiriki uzinduzi wa Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia na Kuendeleza Misitu ya Mikoko ambapo Mgeni Rasmi alikuwa ni Waziri wa Maliasili mHE. Balozi Pindi Chana katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Agosti 05, 2025, Mhe. Balozi Waziri Pindi Chana alisema Mikoko ni nyara ya Serikali inayotakiwa kulindwa kutokana na umuhimu wake kwa jamii na mazingira.
“Mikoko ni uti wa mgongo wa uhai wa Bahari ya Hindi. Huchuja taka, huzuia mmomonyoko wa fukwe, ni hifadhi ya kaboni, na ni mazalia ya samaki. Kuiacha iharibiwe ni kuhatarisha maisha ya watu na viumbe,” alisema Waziri Chana mbele ya viongozi wa serikali, wanadiplomasia na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.
Waziri Chana alibainisha kuwa Tanzania ina zaidi ya hekta 158,100 za mikoko zinazosambaa katika wilaya 14 za ukanda wa Pwani. Hata hivyo, rasilimali hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uvamizi wa maeneo, ujenzi holela, uchimbaji wa mchanga na uchafuzi wa mazingira.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Waziri Chana alisisitiza taasisi husika zichukue hatua mahsusi zifuatazo: Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kushirikiana na mamlaka nyingine katika kulinda na kusimamia mikoko; taasisi za utafiti kufanya tafiti zenye mwelekeo wa matumizi endelevu ya rasilimali hiyo; Wizara kushirikiana na sekta ya utalii kubadilisha mikoko kuwa vivutio vya kiutalii; na wadau wa maendeleo kuendelea kutoa msaada wa kifedha, kitaalamu na kiufundi ili kufanikisha utekelezaji wa mkakati huo kwa ufanisi.
Kwa upande wa TFS, Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo, alisema mkakati huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa karibu na wadau wa ndani na nje ya nchi, na ni nyenzo muhimu ya kulinda ardhi oevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Katika uzinduzi huo wa Mkakati huo, MPRU iliwakilishwa na Mhifadhi Mfawidhi kutoka Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingiliano ya Mto Ruvuma (MBREMP) pamoja na Mhifadhi Mfawidhi, Maria Pentzel.
Mashirika mengine yalishiriki kikamilifu katika uzinduzi wa mkakati huo katika kutoa mchango wa kitaalamu, kifedha na wa kielimu ikiwemo Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Asilia (IUCN), Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), Mtandao wa Uhifadhi wa Ukanda wa Pwani (Mwambao), Shirika la EarthLungs, pamoja na Wetlands International.