MPRU YATANGAZA FURSA ZA UTALII WA BAHARI KWA WANAFUNZI WA SoAF-UDSM
MPRU YATANGAZA FURSA ZA UTALII WA BAHARI KWA WANAFUNZI WA SoAF-UDSM

Jumatatu, Aprili 20, 2026, Dar es Salaam

Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) imekutana na wanafunzi 41 wa Shule Kuu ya Sayansi ya Akua na Teknolojia ya Uvuvi – Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SoAF), kwa lengo la kutangaza fursa mbalimbali za utalii wa bahari zilizopo nchini na kuhamasisha utalii wa bahari katika maeneo ya uhifadhi pamoja na vivutio vyake vya kipekee ilipotembelea chuo hicho leo Aprili 20, 2026 kilichopo Kunduchi jijini Dar es Salaam. 

Mawasilisho hayo yaliongozwa na Afisa Masoko, Bi. Halima Tosiri, kwa kushirikiana na Afisa Maendeleo ya Jamii, Bw. Kululetela Lukandiga, pamoja na Mhifadhi Bahari, Bw. Romanius Ruhinda kwa kuwatangazia wanafunzi hao kuhusu vivutio vya utalii wa bahari, ikiwemo miamba ya matumbawe, fukwe za kuvutia, viumbe hai wa baharini pamoja na mandhari ya kipekee ya maeneo ya hifadhi, na namna vinavyoweza kuchangia ukuaji wa uchumi na ajira.

Aidha, wanafunzi hao walipata fursa ya kufahamu mbinu bora za kujiajiri kupitia shughuli za uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, ikiwemo kilimo cha mwani, uhifadhi na upandaji wa mikoko, pamoja na shughuli nyingine zinazolenga kulinda mazingira ya bahari huku zikichangia kuongeza kipato.

Halikadhalika, wanafunzi hao walisisitizwa umuhimu wa ushiriki wa vijana katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za bahari, ili kuhakikisha zinatumika kwa tija kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.