NAIBU KATIBU MKUU, OR - KAZI, UCHUMI NA UWEKEZAJI ZANZIBAR ASISITIZA UMUHIMU WA KUTUNZA MIAMBA YA MATUMBAWE KWA KUWA INACHANGIA UKUAJI WA UCHUMI NCHINI
NAIBU KATIBU MKUU, OR - KAZI, UCHUMI NA UWEKEZAJI ZANZIBAR ASISITIZA UMUHIMU WA KUTUNZA MIAMBA YA MATUMBAWE KWA KUWA INACHANGIA UKUAJI WA UCHUMI NCHINI

Ijumaa, Julai 25, 2025, Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Dkt. Rashid Ali Salim, amesisitiza umuhimu wa kulinda miamba ya matumbawe kwa kuwa inachangia ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuvutia watalii kutoka kote duniani.

Aliyasema hayo Julai 22, 2025 wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kitaifa wa Uhifadhi wa Miamba ya Matumbawe Imara (NAPCRCR) uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano katika Hoteli ya Peacock iliyopo jijini Dar es Salaam na kueleza matarajio yake kuwa utekelezaji wa mpango huo utatatua changamoto mbalimbali zinazokumba Hifadhi za Bahari, ikiwemo uvuvi haramu, mabadiliko ya tabianchi pamoja na uharibifu wa mazingira.

“Ingawa nchi inanufaika sana kupitia utalii mkubwa, ustawi wa kiikolojia, usalama wa chakula, biashara, uwekezaji, na ustawi wa jamii za pwani, ili tuweze kufaidika kikamilifu na hifadhi zetu za baharini, changamoto hizi lazima zitatuliwe,” alisema Dkt. Rashid Ali Salim.

Naye kwa upande wake, Mratibu wa Mradi ambaye pia ni Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU), Bw. Godfrey Ngupula, alieleza kuwa hali ya miamba ya matumbawe nchini bado ni nzuri, japokuwa katika miaka ya karibuni ilikumbwa na athari kubwa kutokana na uvuvi wa mabomu.

“Tuna jukumu la kulinda rasilimali zetu; kuharibu miamba ya matumbawe kunaweza kudhoofisha uchumi wa jamii za pwani na mapato ya taifa ambayo kwa kiasi kikubwa yanategemea miamba ya matumbawe. Hivyo, kuanzishwa kwa mpango huu wa kimkakati kutaimarisha ulinzi wa maeneo haya,” alisema Bw. Ngupula.

Halikadhalika, Bw. Ngupula alieleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wavuvi wadogo katika maeneo ya pwani wanategemea rasilimali kutoka kwenye miamba ya matumbawe, huku Tanzania ikikadiriwa kupata mapato ya takribani dola za Kimarekani bilioni 14 kutoka kwenye rasilimali hizo.