NAIBU WAZIRI OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA ATEMBELEA BANDA LA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVU NA TAASISI ZAKE

Alhamisi, June,05, 2025, Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. khamis Hamza Khamis ametembelea Banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Taasisi zilizopo chini yake kwa lengo la kufanya Ukaguzi kuhusu elimu inayotolewa na Wizara pamoja na Taasisi zake kwenye maonyesho Juni 04, 2025 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Aidha, Taasisi zilizoshiriki kwenye maonyesho hayo ni pamoja na Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari kuu (DSFA),Bodi ya Nyama, Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO), Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA),Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) pamoja na Maabara ya Taifa ya Uvuvi.
Akizungumza katika Maonesho hayo, Mfahidhi Bahari kutoka MPRU, Gister Nkini alisema wananchi wategemee kupata elimu ya utunzwaji wa mazingira ya Bahari pamoja na elimu ya kufanya urejeshaji wa Rasilimali za Bahari pamoja na urejeshaji wa taka za plastiki.
“Kazi zetu kubwa kwenye kuhifadhi bahari na kutunza mazingira ya bahari ni kufatilia rasilimali za bahari kama mikoko, matumbawe na nyasi bahari pia kufanya usafi wa fukwe zilizopo ndani ya uhifadhi kwa kuzikusanya, kuzichambua na kuzipelekea kwa wadau mbalimbali wanaofanya kazi za urejeshaji” alisema Gister Nkini.
Halikadhalika, aliongeza kuwa wao hufanya zoezi za urejeshwaji wa rasilimali za bahari zilizoharibika ikiwemo mikoko, matumbawe na nyasi bahari na kufanya doria kwaajili ya kutokomeza uvuvi haramu ambao sio endelevu katika maeneo ya Hifadhi.