SERIKALI YADHAMIRIA KUHAKIKISHA MAFIA INAPIGA HATUA UCHUMI WA BULUU
Jumatatu, Disemba 16, 2024 Mafia
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Ndg. Rashid Mchatta amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Wilaya ya Mafia inapiga hatua katika masuala ya uchumi wa buluu akifananisha juhudi hizo na mafanikio yaliyopatikana Zanzibar.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani ameyasema hayo alipokuwa akihutubia katika uzinduzi wa Kongamano la Uwekezaji Katika Uchumi wa Buluu Wilaya ya Mafia lililofanyika Disemba 07, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Chicco.
"Mafia ni hazina ya kipekee yenye rasilimali nyingi zinazoweza kuinua uchumi wa wakazi wake na taifa kwa ujumla. Ni jukumu letu, kama wadau wa maendeleo, kuhakikisha tunatumia fursa hizi kwa njia endelevu na yenye manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho," alisema Mchatta.
Aidha, Mchatta alibainisha kuwa uchumi wa buluu una nafasi kubwa katika kuleta maendeleo endelevu kupitia uvuvi, utalii na uhifadhi wa mazingira ya bahari.
Kongamano hilo limewakutanisha viongozi wa serikali, wadau wa uvuvi, mazingira, na utalii kutoka taasisi mbalimbali, wakiwemo wajumbe wa Bodi ya Utalli Tanzania. Bodi hiyo iliwakilishwa na Mwenyekiti wake, Dkt. Ramadhan Dau, pamoja na Mkurugenzi wa Bodi, Bw. Ephraim Mafuru, ambao walieleza dhamira yao ya kushirikiana na wadau katika kukuza sekta ya utalii wilayani Mafia.
Naye kwa upande wake, Mhifadhi Mfawidhi kutoka Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia (MIMP) Bw. Amin Abdallah kutoka Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) alishiriki kikamilifu katika kongamano hilo.
Aidha, Kongamano hilo lilibua mijadala juu ya mbinu bora za kuvutia uwekezaji katika sekta za uvuvi wa kisasa, utalli endelevu, na uhifadhi wa mazingira ya bahari, huku washiriki wakisisitiza umuhimu wa kushirikiana kuimarisha uchumi wa Wilaya hiyo kupitia rasilimali za bahari.