SHIRIKA LA MAENDELEO LA UFARANSA (AFD) LAFANYA ZIARA DMRS
Jumanne, Februari 03, 2026. Dar es Salaam

Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) kupitia Kituo cha Dar es Salaam Marine Reserves System (DMRS) imepokea ugeni wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) uliofanya ziara katika maeneo mbalimbali yanayohifadhiwa jijini Dar es Salaam na kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo Umoja wa Wavuvi kwenye Mwalo wa Kunduchi, Umoja wa BMU Kunduchi pamoja na Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mbudya.
Ziara hiyo imelenga kubaini changamoto zinazokabili juhudi za uhifadhi katika maeneo yanayohifadhiwa (MPAs) pamoja na kuangazia maeneo ya ushirikiano yatakayowezesha utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na changamoto hizo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Idara ya Uhifadhi Makao Makuu ya MPRU, Ndg. Godfrey Ngupula, pamoja na Afisa Utalii wa Kituo cha DMRS, Ndg. Sifuni Sispatery, walieleza kwa kina juu shughuli za uhifadhi, ushirikishwaji wa jamii za pwani katika usimamizi wa rasilimali za bahari pamoja na fursa za uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu zilizopo katika maeneo yanayohifadhiwa.
Kupitia ziara hiyo, AFD ilipata fursa ya kujifunza kwa karibu namna MPRU inavyotekeleza uhifadhi shirikishi kwa kushirikiana na jamii za pwani na wadau wengine katika maeneo mbalimbali ya uhifadhi.

