TACMP INASHIRIKI MAONESHO YA 12 YA BIASHARA NA UTALII TANGA
TACMP INASHIRIKI MAONESHO YA 12 YA BIASHARA NA UTALII TANGA

Jumanne, Juni 03, 2025, Tanga

Hifadhi ya Bahari ya Silikanti Tanga (TACMP) inashiriki katika Maonesho ya 12 ya Biashara na Utalii yanayofanyika katika Viwanja vya Mwahako katika Mkoa wa Tanga.

Maonesho hayo yaliyoanza kuanzia Mei 28 hadi Juni 6, 2025, ambapo Mgeni Rasmi ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian.

Akizungumza katika ufunguzi rasmi wa Maonyesho ya 12 ya Biashara na Utalii yanayoendelea jijini Tanga, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian amesema mkoa huo umejipanga kikamilifu kuweka mazingira bora ya uwekezaji.

Hotuba ya Mhe Balozi Dkt Batilda, imetolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe Dadi Kolimba, akisema mkoa una maeneo mengi yenye mvuto kwa uwekezaji, hususan katika sekta ya viwanda, na kwamba juhudi zinaendelea kuboresha miundombinu ya msingi ikiwemo barabara, maji, umeme na huduma za mawasiliano.

“Tunawahamasisha wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na taasisi za umma na binafsi kutumia maonyesho haya kama jukwaa la kujifunza, kushirikiana na kutangaza bidhaa na huduma zao,” amesema.

Aidha, Afisa Utalii wa TACMP, Jamal Mvungi kwa kushirikiana na Afisa Utalii wa TMRS, Happiness Urio waliongoza ushiriki katika Maonesho hayo kwenye Banda kwa kunadi utalii wa Bahari, kuhamasisha kutembelea maeneo ya Uhifadhi na  kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na shughuli za Uhifadhi.

Serikali ya Mkoa imeahidi kuendelea kuimarisha mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla. Maonesho hayo ya 12 ya Biashara na Utalii yalibeba Kauli Mbiu isemayo, "Mwonekano wa Wadau Sekta ya Umma na Binafsi kwenye Uwekezaji, Ukuaji na Uendelevu wa Biashara".