TACMP, TMRS ZAFANYA ZIARA YA UHAMASISHAJI VYUO VYA TANGA KUKUZA UELEWA WA UHIFADHI WA BAHARI
Jumanne, Mei 05, 2026, Tanga
Hifadhi ya Bahari Tanga Silikanti (TACMP) kwa kushirikiana na Tanga Marine Reserves System (TMRS), imefanya ziara ya uhamasishaji katika vyuo mbalimbali mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuelimisha jamii, hususan wanafunzi, kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali za bahari na fursa zilizopo katika sekta hiyo.
Ziara hiyo iliyofanyika Mei 05, 2026 ilihusisha kutembelea Chuo cha Utumishi wa Umma – Kampasi ya Tanga pamoja na Chuo cha Utalii cha Masai. Lengo lilikuwa ni kujitangaza, kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira ya bahari, na kuhamasisha ushiriki wa vijana katika utalii wa bahari.
Akizungumza katika ziara hiyo, Afisa Utalii Bw. Jamal Mvungi ameeleza kuwa taasisi hizo zinaendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii ili kulinda rasilimali za bahari kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo, akisisitiza nafasi ya vyuo katika kufikia vijana.
Kwa upande wake, Afisa Utalii Bi. Happiness Orio amebainisha kuwa sekta ya utalii wa bahari ina fursa nyingi za ajira na kujiajiri, zikiwemo uongozaji watalii, shughuli za uhifadhi, na huduma mbalimbali za utalii.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Bi. Joyce Mziray amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za uhifadhi na jamii, huku Mhifadhi Bahari Bi. Jenipher Julias amewataka viongozi kuwasisitiza wanafunzi kutumia elimu yao kulinda mazingira ya bahari.
Vilevile, walijadiliana pia njia bora za kushirikiana katika kuendeleza elimu ya uhifadhi na kukuza utalii wa bahari na kuweka mikakati ya kuwashirikisha vijana katika shughuli za utalii wa bahari.

