TACMP YAPOKEA UGENI KUTOKA GHANA KWA ZIARA YA MAFUNZO
Ijumaa, Juni 26, 2026, Tanga
_1782791227.jpeg)
Hifadhi ya Bahari ya Tanga Silikanti (TACMP) imepokea wageni 20 kutoka nchini Ghana waliokuwa katika ziara ya mafunzo (Study Tour Visit) iliyofanyika kuanzia Juni 24 hadi 26, 2026 Mkoani Tanga. Wageni hao walijumuisha wawakilishi kutoka Serikalini, Wahadhiri na Maprofesa wa vyuo vikuu, wawakilishi wa jamii pamoja na wachakataji wa mazao ya uvuvi (Fish processors), ukiwa na lengo la kujifunza uzoefu wa Tanzania katika usimamizi wa Maeneo Tengefu ya Baharini (Marine Protected Areas).
Katika ziara hiyo, wageni walipata fursa ya kujifunza mifumo mbalimbali ya usimamizi wa Maeneo Tengefu ya Baharini, ikiwemo mbinu za uhifadhi wa rasilimali za bahari, ushirikishwaji wa jamii katika shughuli za uhifadhi pamoja na mikakati inayotekelezwa na TACMP kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
Aidha, wageni hao walitembelea mtaa wa Geza uliopo ndani ya eneo la hifadhi katika Jiji la Tanga, ambapo walijifunza shughuli za uhifadhi wa misitu ya mikoko na namna Kamati za Uhusiano za Vijiji (Village Liaison Committees – VLCs) zinavyoshirikiana na Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) katika kulinda rasilimali za bahari. Wageni hao pia walitembelea maeneo ya baharini yanakotekelezwa shughuli za urejeshwaji wa miamba ya matumbawe (Coral Reef Restoration) na kujionea hatua mbalimbali zinazochukuliwa kurejesha afya ya mifumo ikolojia ya bahari.
Katika hatua nyingine, ujumbe ulifika Kijiji cha Moa, Wilaya ya Mkinga, na kujionea shughuli mbadala za kiuchumi zinazotekelezwa na jamii kwa kushirikiana na Wildlife Conservation Society (WCS). Kupitia mradi huo, wananchi wamewezeshwa kuongeza thamani ya zao la mwani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo biskuti, unga wa mwani na cookies, hatua inayochangia kuongeza kipato na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za bahari.
Ziara hiyo imeendelea kuonesha nafasi ya MPRU kama kitovu cha kujifunza mbinu bora za usimamizi wa maeneo Tengefu ya baharini barani Afrika, huku ikiimarisha ushirikiano wa kimataifa na kubadilishana uzoefu katika uhifadhi wa mazingira ya bahari na maendeleo endelevu ya jamii zinazozunguka maeneo ya Hifadhi.

