TACMP YASHIRIKI MAONESHO YA BIASHARA YA TANGA TRADE FAIR 2026
TACMP YASHIRIKI MAONESHO YA BIASHARA YA TANGA TRADE FAIR 2026

Jumatano, Juni 03, 2026, Tanga

Hifadhi ya Bahari ya Tanga Silikanti (TACMP) imeshiriki kikamilifu katika Maonesho ya Biashara ya Tanga Trade Fair 2026 yanayofanyika katika Viwanja vya Mwahako, Jijini Tanga. Maonesho hayo yalianza tarehe 28 Mei 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 6 Juni 2026, yakikusanya taasisi mbalimbali za umma na binafsi kwa lengo la kuonesha huduma, bidhaa na mchango wao katika maendeleo ya taifa.

Aidha, tarehe 2 Juni 2026, banda la Hifadhi ya Bahari ya Tanga Silikanti lilipata fursa ya kutembelewa na Mgeni Rasmi wa maonesho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mheshimiwa Ayubu Yasin Sebabile, ambaye alizindua rasmi maonesho hayo. Katika ziara yake, Mheshimiwa Sebabile alipongeza juhudi zinazofanywa na taasisi mbalimbali, ikiwemo TACMP, katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania kupitia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika uhifadhi wa rasilimali za asili kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Kupitia ushiriki huo, Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (Tanga) imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, ikiwemo miamba ya matumbawe, nyasi bahari, mikoko na viumbe mbalimbali wa baharini. Elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa jamii juu ya mchango wa rasilimali za bahari katika kukuza uchumi wa buluu, kuimarisha maisha ya wananchi na kuhakikisha rasilimali hizo zinahifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Timu ya wataalamu kutoka TACMP inayoongozwa na Afisa Utalii, Bw. Jamal Mvungi, na Afisa Masoko, Bi. Happiness Urio, imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu na kujibu maswali ya wananchi wanaotembelea banda la taasisi hiyo. Kupitia mawasiliano ya ana kwa ana, wananchi wamepata fursa ya kujifunza kuhusu shughuli za uhifadhi, fursa za utalii wa baharini pamoja na mchango wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

slot gacor