UHIFADHI WA MIAMBA YA MATUMBAWE NI NGUZO MUHIMU YA UCHUMI WA BULUU TANZANIA - DKT. SWEKE
Jumanne, Mei 26, 2026, Kibaha - Dar es Salaam

Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika juhudi za kulinda miamba ya matumbawe dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia Mradi wa Global Environment Facility–Coral Reef Rescue Initiative (GEF-CRRI), unaotekelezwa kwa lengo la kuhifadhi mifumo ikolojia ya baharini na kuimarisha ustawi wa jamii za mwambao.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Uongozi wa mradi huo kilichofanyika Mei 26, 2026 Kibaha, Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Dkt. Emmanuel Andrew Sweke, alisema mradi huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa buluu nchini. Alibainisha kuwa miamba ya matumbawe ni makazi muhimu ya viumbe wengi wa baharini na maeneo ya kuzaliana kwa samaki, hivyo juhudi za uhifadhi na urejeshaji wake ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya sekta ya bahari. Aliongeza kuwa mafanikio yanayoonekana katika urejeshaji wa miamba ya matumbawe katika eneo la Mnazi Bay yanaonesha matokeo chanya ya ushirikiano kati ya serikali, wadau wa maendeleo na jamii za mwambao.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa GEF-CRRI, Bw. Godfrey Ngupula, alisema mradi huo wa miaka minne wenye thamani ya dola za Marekani 900,000, uliozinduliwa mwaka 2023 chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, unalenga kuimarisha uhifadhi na usimamizi endelevu wa miamba ya matumbawe ili kuongeza uwezo wake wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Alisema tafiti zinaonyesha baadhi ya matumbawe yaliyopo Tanzania yana uwezo mkubwa wa kustahimili ongezeko la joto la bahari na uchafuzi wa mazingira, jambo linalotoa fursa ya kuendelea kuyahifadhi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Naye Mratibu wa Programu wa Shirika la Uhifdhi wa Mazingira Duniani (WWF), Dkt. Modesta Medard, alisema Tanzania imepiga hatua muhimu katika utekelezaji wa mradi huo, ikiwemo kuanzishwa kwa Kituo cha Kitaifa cha Miamba ya Matumbawe (NCRH), urejeshaji wa maeneo yaliyoharibiwa pamoja na kuimarishwa kwa ushirikiano wa wadau kupitia miongozo na mifumo mbalimbali ya usimamizi. Alisema hatua hizo zinaendelea kuimarisha uwezo wa nchi katika kulinda na kuhifadhi mifumo ya ikolojia ya baharini inayokabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

