USAFI WA KISIWA CHA JAMBE KUFUNGUA MILANGO YA UTALII TACMP
USAFI WA KISIWA CHA JAMBE KUFUNGUA MILANGO YA UTALII TACMP

Hifadhi ya Bahari ya Tanga Silikanti (TACMP) kwa kushirikiana na Kamati Ndogo ya Uhifadhi ya Sahare (VLC Sahare) imekamilisha zoezi la usafi katika Kisiwa cha Jambe, Tanga, likiwa na lengo la kufungua vivutio vya utalii na kulinda mazingira ya baharini.

Hatua hii inakuja kufuatia ziara iliyofanywa Agosti 25, 2025 na Kaimu Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania Bw. Davis Mpotwa kwa kutembelea Kisiwa cha Jambe akiwa ameambatana na watumishi wa TACMP akiwemo Bw. Mvungi, David Kabodo na Joyce Mziray ambapo ziara hiyo ililenga kuanzisha shughuli za Utalii katika Kisiwa cha Jambe.

Zoezi la usafi lilifanyika Agosti 30-31, 2025, likihusisha wanakamati 13 wa VLC Sahare na wakazi watatu wa eneo hilo. Takribani shilingi milioni 1.62 zilitumika kununua vifaa vya usafi, sare na posho za washiriki.

Mwenyekiti wa VLC Sahare, Bw. Jumaa Mbwana na timu yake ilifanikiwa kufungua njia vinjari katika maeneo ya kihistoria kama mnara wa enzi za ukoloni, visima na mashamba ya kale.

Aidha, Ripoti ya TACMP inaeleza kuwa eneo maalum limechaguliwa kwa ajili ya ujenzi wa mabanda ya utalii yanayoangalia Bahari ya Hindi na Jiji la Tanga.

Hata hivo, changamoto ya upungufu wa nguvu kazi na utegemezi wa kazi za kujitolea imetajwa kuathiri ufanisi wa usafi huo.

TACMP imependekeza kufanyika kwa usafi wa nyongeza, kutafuta wawekezaji na kuweka alama za maelekezo kwenye njia vinjari, ili kuboresha zaidi mandhari ya kisiwa hicho chenye vivutio vya kiasili na kihistoria.

Usafi wa eneo la juu mwamba ambapo mabanda yatajengwa.

 

Muonekano wa mabanda baada ya kusafishwa.

 

Utengenezaji wa njia ya kuingia ndani ya Kisiwa kutoka upande wa pili na mashambani.