WAHIFADHI BAHARI NA WANAJAMII WA MAFIA WAHITIMISHA MAFUNZO YA UKUFUNZI WA UREJESHWAJI WA MATUMBAWE NCHINI INDONESIA

Alhamis Octoba 02, 2025 Dar es Salaam
Watumishi wa Marine Parks and Reserves Unit (MPRU) pamoja na wanajamii kutoka Kisiwa cha Mafia wamemaliza mafunzo ya wiki nne ya urejeshwaji wa matumbawe yaliyofanyika katika eneo la Raja Ampat, Indonesia. Mafunzo haya yaliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Ropes of Hope kwa lengo la kuongeza ujuzi wa kitaalamu na uwezo wa ukufunzi kwa washiriki kutoka Tanzania.
Katika kipindi cha mafunzo, washiriki walihusishwa moja kwa moja kwenye kazi za vitendo za kurejesha matumbawe, zikiwemo mbinu za upandaji, ufuatiliaji na usimamizi wa miamba ya bahari. Matokeo ya moja kwa moja ni pamoja na usimikaji wa miundo ya kusaidia ukuaji wa matumbawe kama metal spiders, mesh na rope nursery, pamoja na upandaji wa zaidi ya vipande 700 vya matumbawe katika maeneo ya Sapokren, Davang na Yenbekwan. Vilevile, vitalu vya matumbawe (nurseries) vilianzishwa na kupandwa zaidi ya vipande 3,000 huku viumbe waharibifu wa miamba (crown-of-thorns starfish) 82 wakiondolewa ili kulinda afya ya matumbawe.
Akizungumzia mafunzo hayo, Mhifadhi Bahari wa MPRU, Pashcal Mkongola, alisema, “Ujuzi huu ni wa kipekee kwa Tanzania. Sasa tunaweza kutumia mbinu za kiteknolojia tulizojifunza kwa ufanisi zaidi katika urejeshwaji wa matumbawe, na muhimu zaidi, tumepata uwezo wa kufundisha na kushirikisha wengine.”
Kwa upande wao, wanajamii waliowakilisha Mafia, Mikidadi Ahmadi na Hatibu Sheshe, walisema mafunzo yamewapa mwamko mpya wa kushirikiana na jamii zao kulinda rasilimali za bahari. Mikidadi alisema, “Tutatumia ujuzi huu kuelimisha na kushirikiana na wavuvi na wanajamii wenzetu kwa ajili ya maisha endelevu ya pwani.”
MPRU inatarajia kuwa ujuzi walioupata washiriki utaleta manufaa makubwa katika kuendeleza juhudi za uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari nchini. Kupitia nafasi yao ya sasa kama wakufunzi, washiriki hao watakuwa chachu ya mabadiliko kwa kuwajengea uwezo wataalamu wa uhifadhi na jamii za pwani, hivyo kuongeza wigo wa ushiriki na kuimarisha uwajibikaji wa pamoja katika kulinda mazingira ya baharini.