WANAFUNZI 140 WA SUA WATEMBELEA TACMP
Jumapili, Mei 17 2026, Tanga
Hifadhi ya Bahari ya Silikanti Tanga (TACMP) imepokea ugeni wa wanafunzi 140 kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wakiongozwa na mhadhiri wao, Profesa Nsajigwa Mbije. Ziara hii imefanyika kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo, ikilenga kuwajengea uelewa kuhusu shughuli za uhifadhi wa mazingira ya bahari.
Katika ziara hiyo, wanafunzi walipata fursa ya kujifunza namna uhifadhi unavyotekelezwa, ikiwemo utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali, pamoja na mbinu za ushirikishaji jamii katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za bahari.
Aidha, walipatiwa elimu kuhusu utalii wa baharini ambapo walielezwa vivutio vinavyopatikana ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa na fursa za uwekezaji zilizopo. Sambamba na hilo, walifahamishwa namna shughuli za utalii zinavyosaidia kupatikana kwa mapato na kuchangia katika kukuza uchumi kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
Elimu hiyo ilitolewa na Mhifadhi Mfawidhi Bi. Magreth Mchome kwa kushirikiana na timu ya wataalamu wa TACMP, Ambapo wamewaimiza wanafunzi kuendelea kuwa mabalozi wa uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
Ziara hii imekuwa chachu ya kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali za bahari na nafasi ya sekta ya utalii katika kukuza uchumi wa buluu. Pia imewahamasisha kuendeleza juhudi za taifa katika kulinda rasilimali za bahari kupitia taaluma zao na ushiriki wao katika jamii.

