WANAFUNZI NIT WAHAMASISHWA KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII KATIKA HIFADHI ZA BAHARI
Jumanne, Aprili 28, 2026, Dar es Salaam
Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania ((MPRU) kupitia wataalam wake wamehamasisha wanafunzi 400 kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kutembelea Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu nchini ili kuongeza uelewa wao kuhusu vivutio vya baharini na fursa zilizopo katika sekta ya utalii wa bahari.
Uhamasishaji huo uliongozwa na Afisa Maendeleo ya Jamii Bw. Kululetela Lukandiga pamoja na Mhifadhi Bahari Bw. Rashid Kilawi tarehe 28, Aprili 2026 katika ziara hiyo chuoni hapo Mabibo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwafikia vijana na kuwahamasisha kushiriki katika utalii na uhifadhi wa rasilimali za bahari.
Wataalam hao walieleza kwa kina kuhusu umuhimu wa Hifadhi za Bahari na kama kivutio kikubwa cha utalii, wakibainisha uwepo wa viumbe hai wa aina mbalimbali, miamba ya matumbawe pamoja na fukwe zenye kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi.
Aidha, wanafunzi walihamasishwa kutumia fursa zilizopo kujipatia kipato kupitia shughuli rafiki kwa mazingira kama vile kilimo cha mwani, utunzaji wa mikoko na huduma za utalii, huku wakizingatia misingi ya uhifadhi endelevu wa rasilimali za bahari.
Halikadhalika, wanafunzi hao waliaswa kuwa mabalozi wa uhifadhi kwa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira ya bahari, ili kuhakikisha rasilimali hizo zinaendelea kuwa na manufaa kwa taifa sasa na baadaye.

