WARSHA YA KUBUNI MKAKATI WA USHIRIKIANO NA MAWASILIANO MAALUM MRADI WA CRRI

Jumatano, Mei 28, 2025, Dar es Salaam
Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) kupitia Mratibu wa Mradi wa Uokoaji wa Miamba Matumbawe (CRRI) na Mhifadhi Mkuu wa MPRU Bw. Godfrey Ngupula wamefungua warsha ya siku tatu (Mei 28-30, 2025) ya kubuni mkakati wa ushirikiano na mawasiliano maalum kwa ajili ya mradi wa Coral Reef Rescue Initiative National Hub nchini Tanzania.
Warsha hiyo inayofanyika katika Hoteli ya Peacock iliyopo Dar es Salaam, inaongozwa na Wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Queensland kutoka nchini Australia na kuwaleta pamoja wataalamu wa mawasiliano kutoka Tanzania na Madagascar kukuza ushirikiano wa Kimataifa na kubadilishana maarifa.
Malengo muhimu ya warsha hii ni pamoja na kuunda mkakati wa mawasiliano na ushirikiano maalum kwa CRRI National Hub, kutengeneza mpango wa utekelezaji unaoweza kufuatiliwa kwa ufanisi, kuimarisha uwezo wa washiriki katika kutekeleza na kuhamasisha mkakati huo kwa ufanisi.
Aidha, jitihada zinazofanywa na MPRU katika kuimarisha mifumo ya mawasiliano ni moja ya hatua muhimu katika kulinda na kurejesha mifumo muhimu ya mazingira ya Miamba ya Matumbawe kwa vizazi vijavyo.