WATALII 218 WA KUTOKEA MATAIFA MBALIMBALI WATEMBELEA KISIWA CHA SINDA, WAVUTIWA NA MANDHARI YA KISIWA HICHO
Jumanne, Aprili 07, 2026, Dar es Salaam

Watalii takribani 218 kutokea nchi mbalimbali duniani Aprili 07, 2026 wametembelea Kisiwa cha Sinda kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam katika ziara ya kitalii wakitokea nchini Msumbiji.
Watalii hao walifika kutembelea Kisiwa hicho na Meli ya Kimaitaifa iitwayo ‘Silver Cloud’ wametembelea Kisiwa cha Sinda na kuvutiwa na mandhari ya kipekee pamoja na vivutio vya asili vinavyopatikana katika kisiwa hicho.
Afisa Utalii kutoka DMRS Bw. Sifuni Sospatery amewakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika utalii wa Bahari ili kuchochea ongezeko la idadi ya watalii nchini.
“Tunakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika restaurant, migahawa pamoja na bar lakini tunakwenda mbali zaidi katika uwekezaji wa malazi kwani maeneo yetu yanavutia zaidi watu kulala baharini kwahiyo watu wanakaribishwa kuja kuwekeza katika ikolojia katika visiwa vyetu; Alisema Bw. Sifuni.
“Watalii hulipa ada ya kuingia katika maeneo ya hifadhi, ambapo wageni wanaotoka Afrika Mashariki hutozwa Shilingi 11,800 kwa siku, huku wageni kutoka nje ya mataifa ya Afrika Mashariki hutozwa Shilingi 47,500 kulingana na thamani ya fedha za kigeni kwa siku husika; Aliongezea Sifuni.
Kwa upande wake, Mhifadhi wa Bahari kutoka DMRS, Bi. Catherine Msina, alitoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa rasilimali za bahari ili kuhakikisha uendelevu wa sekta ya utalii.
“Shughuli zetu kuu ni kulinda mazingira ya bahari kwa kuhakikisha maeneo haya yanabaki salama na hakuna uvuvi haramu unaofanyika. Hii inasaidia kuhifadhi rasilimali za bahari na kuvutia watalii wengi zaidi,” alisema Bi. Msina.
Aliongeza kuwa Kisiwa cha Sinda kina vivutio vya kipekee vikiwemo fukwe safi, mazingira mazuri ya kuogelea pamoja na mti wenye umbo la chupa ya champagne ambao huwavutia wageni wengi.
Nao watalii waliotembelea Kisiwa hicho wamefurahia uzuri wa mazingira wakitaja fukwe safi, maji mazuri (blue crystal-clear water), mifumo mizuri ya ikolojia iliyowawezesha kuona aina mbalimbali ya samaki.


