WATUMISHI WA MPRU WASHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI

Ijumaa, Mei 02, 2025, Dar es Salaam
Watumishi wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU) wameungana na wafanyakazi wengine duniani kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), ambayo kwa mwaka huu yameadhimishwa kitaifa katika Mkoa wa Singida, yakiongozwa na Mgeni Rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo “Uchaguzi Mkuu 2025 utuletee viongozi wanaojali haki na maslahi ya wafanyakazi, sote tushiriki,” ikisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wafanyakazi katika mchakato wa uchaguzi kwa ajili ya mustakabali bora wa haki zao.
Mhe. Rais Dkt. Samia akihutubia katika kilele cha sherehe hizo, ametangaza habari njema kwa wafanyakazi wote nchini kwa kutangaza ongezeko la kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 35, hatua inayolenga kuboresha maisha ya mfanyakazi na kutambua mchango wao katika ujenzi wa taifa.
Maadhimisho ya Mei Mosi yameendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam, maadhimisho hayo yamefanyika kwa mafanikio makubwa yakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Albert Chalamila.
Baadhi ya watumishi kutoka MPRU wakiongozwa na Mhifadhi Mfawidhi wa DMRS Bi. Anitha Julius (katikati) wakiwa katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watumishi kutoka Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia (MIMP) wakiwa njiani kuelekea katika viwanja vya Ofisi za Halmashauri, Chicco katika Wilaya ya Mafia kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.
Baadhi ya watumishi kutoka Hifahi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingiliano ya Mto Ruvuma (MBREMP) wakiwa katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani katika Viunga vya Sabasaba vilivyopo katika Wilaya ya Newala, Mkoani Mtwara.