WCS YAKABIDHI MIRADI YA UKARABATI WA OFISI NA UNUNUZI WA VIFAA TCMP
WCS YAKABIDHI MIRADI YA UKARABATI WA OFISI NA UNUNUZI WA VIFAA TCMP

Alhamis, Aprili 17, 2026, Tanga

Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania (MPRU), Dkt. Emmanuel Sweke amepokea ukarabati wa jengo la ofisi pamoja na ununuzi wa vifaa mbalimbali katika Kituo cha Hifadhi ya Bahari Silikanti Tanga (TCMP).

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Dkt. Sweke amelishukuru Shirika la Kuhifadhi Wanyamapori (WCS) kwa kufanikisha utekelezaji wa mradi huo uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 380. Amesema maboresho hayo yataongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za baharini.

“Maboresho haya siyo tu yanaimarisha mazingira ya kazi kwa watumishi wetu, bali pia yanaongeza uwezo wetu wa kusimamia rasilimali za bahari kwa ufanisi zaidi. Tunaamini kuwa uwekezaji huu utachochea matokeo chanya katika uhifadhi, uvuvi endelevu pamoja na kukuza utalii  na uwekezaji wa baharini,” amesema Dkt. Sweke.

Aidha, Dkt. Sweke amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na juhudi za pamoja katika shughuli za uhifadhi, akibainisha kuwa ushirikiano huo unahusisha jamii, wadau wa uhifadhi pamoja na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali (NGOs).

Kwa upande wake, Bw. Benjamin Taylor, Meneja wa Mradi wa Blue Action Fund (BAF) chini ya WCS, ameahidi kuendelea kushirikiana na MPRU katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya uhifadhi wa rasilimali za baharini.

Naye Meneja wa Mradi wa WCS, Dkt. Johnson Mshana, amesema kupitia mradi wa BAF wamefanikiwa kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo ukarabati wa jengo la ofisi, ujenzi wa jengo la kuhifadhi boti, ofisi maalum ya utafiti na ufuatiliaji wa rasilimali za baharini zinazotumika katika shughuli za upandaji matumbawe, ujenzi wa njia ya kupitishia boti (slipway), ununuzi wa tela ya kubeba boti, ukarabati wa boti nne pamoja na ununuzi wa injini  mbiliza noti zenye ukubwa wa HP 85 kila moja.

Dkt. Mshana ameongeza kuwa WCS inatarajia kujenga kituo cha habari katika Hifadhi ya Bahari ya Silikanti Tanga kama mwendelezo wa utekelezaji wa mpango kazi katika kituo hicho.

Hafla ya makabidhiano hayo imehudhuriwa na Diwani wa Kata ya Kigombe, wenyeviti na watendaji wa vijiji vya Kigombe na Msakangoto, Afisa Uvuvi kitengo cha doria Tanga, Mwakilishi wa Ofisi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi; Kitengo cha Doria Tanga, Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Muheza pamoja na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Tanga.