ZOEZI LA UREJESHWAJI WA MIAMBA YA MATUMBAWE LAANZISHWA KISIWA CHA MNEMBA

Jumatano, Mei 07, 2025, Zanzibar
Zoezi la pamoja la kuhifadhi mazingira ya Baharini limezinduliwa katika Atolli ya Mnemba, ambapo jumla ya nyota 300 za miamba zimewekwa kwa ajili ya kurejesha miamba ya Matumbawe iliyoathirika.
Zoezi hilo limeongozwa na Linda Bahari kwa kushirikiana na Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu, Dive Point, Mtandao wa Jamii wa Pwani wa Mwambao, Under the Wave, One Ocean, Spanish Dancer Divers na Wavuvi wa maeneo ya karibu.
Nyota hizo za Miamba, zilizoandaliwa kwa vipande vya chuma na kupandikizwa vipande vya matumbawe, zimekusudiwa kuimarisha maeneo yaliyoharibika na kuchochea ukuaji wa Matumbawe, hivyo kuongeza viumbe hai vya Baharini. Hili ni hatua muhimu katika kuimarisha mtandao wa urejeshaji wa miamba katika Bahari ya Hindi Magharibi na usimamizi endelevu wa rasilimali za Baharini.
Malou kutoka Linda Bahari aliongoza operesheni hiyo, akiungwa mkono na Dkt. Makame na Maafisa wa Serikali na kusisitiza kuwa huu si urejeshaji tu bali ni ustahimilivu na kwamba hawapandi Matumbawe bali wanajenga mustakabali.