MTWARA YAAINISHA FURSA ZA UTALII KUVUTIA UWEKEZAJI
Ijumaa, Septemba 4, 2026 Mtwara

Wadau wa uhifadhi, utalii na maendeleo wameainisha fursa mbalimbali za kiuchumi zinazoweza kuchochewa na utalii mkoani Mtwara, huku wito ukitolewa kwa wawekezaji na jamii kuchangamkia fursa hizo ili kuongeza manufaa ya utalii kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa katika mdahalo wa “Unlock Mtwara Destination” ulioandaliwa na Marine Parks and Reserves (MPRU) kupitia jukwaa la Nyangumi Festival 2026, uliowakutanisha wadau muhimu wa sekta hiyo, wakiwemo International Union for Conservation of Nature (IUCN), Tanzania Association of Tour Operators (TATO), wamiliki wa mahoteli na waendeshaji wa huduma za utalii kutoka Mtwara, pamoja na taasisi za fedha na vyombo vya habari, kujadili namna ya kufungua na kukuza uwezo wa Mtwara kuwa kituo cha utalii.
Katika mdahalo huo, fursa zilizotajwa ni pamoja na huduma za usafiri wa majini kwa watalii wanaokwenda kushuhudia vivutio vya baharini, uwekezaji katika malazi na huduma nyingine za utalii, pamoja na nafasi kwa vijana na jamii kushiriki katika shughuli zinazozunguka utalii wa bahari,nchi kavu, malikale, na utamaduni.
Wadau hao pia walisisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa na kuitangaza Mtwara kama eneo lenye vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo utalii wa nyangumi, huku ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, jamii na wadau wa uhifadhi ukitajwa kuwa muhimu katika kugeuza fursa hizo kuwa ajira, biashara na manufaa ya kiuchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

