UJIO WA NYANGUMI MNAZI BAY WAHIMIZA UHIFADHI WA BAHARI
Ijumaa, Septemba 04, 2026 Mtwara
Kila ifikapo kati ya mwezi Julai hadi Novemba Tanzania hufanya tamasha la Nyangumi ambalo msingi wake mkuu ulitokana na tabia ya mnyama huyo kuhamia ukanda wa Hifadhi za bahari za Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma (MBREMP) Iliyopo Msimbati mkoani Mtwara ambao kwa kipindi hicho maji ya bahari katika ukanda huo huwa na asili ya joto.
Katika kipindi hicho Nyangumi ambaye mbali na kuwa na sifa ya kuwa mnyama mkubwa kuliko wote ulimwenguni, anakadiriwa kutembea umbali wa takribani kilomita 8,000 katika kipindi chote cha Mwaka huweka makazi yake katika ukanda huo kwa malengo makuu ambayo ni kutafuta chakula na mazingira salama ya kuzaa na kulea watoto wake.
Uwepo wa tukio hilo sio tu unathibitisha utajiri wa maliasili zinazopatikana nchini bali ni alama ya kudumu inayowakumbusha wananchi wa Mtwara na wengine wote wanaofanya shughuli zao za uvuvi kwenye bahari ya hindi kuendelea kutunza mazingira na kuhifadhi mazalia ya asili ya maeneo hayo ili kuvutia viumbe maji wengi zaidi kufika na kuweka makazi yao nchini katika siku za usoni.
Kwa mujibu wa Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu nchini Dkt. Emmanuel Sweke, Nyangumi ni miongoni mwa wanyama wanaohitaji mazingira tulivu na eneo la Hifadhi la Mnazi bay ni miongoni mwa maeneo yanayobeba sifa hiyo kuanzia pwani hadi majini na hiyo ndo sababu kubwa iliyofanya wachague kuishi hapo kwa kipindi cha miezi 4 kabla ya kuhamia kwingine.
“Tunapoelekea kwenye Dira 2050 ambapo uhifadhi umetiliwa mkazo mkubwa sana tunahimiza wadau mbalimbali ikiwepo sekta binafsi lakini pia Taasisi mbalimbali tushirikiane kwa pamoja kuhifadhi maeneo haya kwani tukihifadhi bahari, tunahifadhi maisha yetu” Amesema Dkt. Sweke.
Tukio hilo ni miongoni mwa shughuli mbalimbali zinazoendelea kuchagiza mchango wa sekta ya Uvuvi kwenye pato la Taifa na ni fursa nyingine ambayo inaendelea kuthibitisha wingi wa fursa zinazopatikana kupitia Uchumi wa Buluu.

