WATUMISHI MPRU WAPATIWA MAFUNZO YA URUBANI WA NDEGE ZISIZO NA RUBANI (DRONE)
Tuesday, 28 July, 2026, Dar es Salaam
Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), kwa kushirikiana na Wakala wa Uswidi wa Usimamizi wa Bahari na Maji (Swedish Agency for Marine and Water Management – SwAM), kupitia programu ya 'SwAM Ocean' inayolenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari nchini Tanzania, imewezesha watumishi wanne kushiriki mafunzo ya urubani wa ndege zisizo na rubani (Drone Pilot Training) yanayofanyika katika Chuo cha Tanzania Civil Aviation Training Centre (CATC), Dar es Salaam, kuanzia tarehe 13 Julai hadi 07 Agosti, 2026.
Watumishi wanaoshiriki mafunzo hayo ni Bw. David Kabodo kutoka Tanga Coelacanth Marine Park (TACMP), Bw. Amosi Singo kutoka Mnazi Bay-Ruvuma Estuary Marine Park (MBREMP), Bw. Benson Amos Mremi kutoka Mafia Island Marine Park (MIMP) na Bw. Jovan Tarimo kutoka Deep Marine Reserves (DMRs), ambao wanapatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo kuhusu uendeshaji salama wa drone kwa kuzingatia kanuni za usafiri wa anga.
Kwa sasa washiriki wanaendelea na mafunzo ya vitendo (Field Practical), ambapo wanatumia maarifa waliyopata darasani kufanya mazoezi ya kurusha drone, ukusanyaji wa taarifa na picha za angani, pamoja na matumizi ya teknolojia hiyo katika ufuatiliaji wa rasilimali za bahari, doria, utafiti na shughuli za uhifadhi.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuimarisha uwezo wa Marine Parks and Reserves Tanzania katika matumizi ya teknolojia ya kisasa kwa ajili ya usimamizi na uhifadhi endelevu wa maeneo tengefu ya bahari, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano kati ya MPRU na SwAM kupitia programu ya SwAM Ocean.

