WADAU WA HIFADHI YA BAHARI MAFIA WAHAMASISHWA MATUMIZI NA USIMAMIZI ENDELEVU WA MAKAZI MUHIMU YA VIUMBE WA BAHARINI
WADAU WA HIFADHI YA BAHARI MAFIA WAHAMASISHWA MATUMIZI NA USIMAMIZI ENDELEVU WA MAKAZI MUHIMU YA VIUMBE WA BAHARINI

Alhamisi Novemba 26, 2026          Mafia

Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) imeendesha warsha ya siku moja leo, tarehe 26 Novemba 2026, kwa wadau wa Hifadhi ya Bahari Mafia kwa lengo la kuhamasisha umuhimi, matumizi na usimamizi endelevu wa makazi muhimu na mifumo ikolojia ya bahari. Warsha hiyo imefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia na kuwakutanisha wadau mbalimbali wanaohusika na uhifadhi na matumizi ya rasilimali za bahari katika eneo la hifadhi.

Miongoni mwa washiriki wa warsha hiyo walikuwa viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa, jamii za wavuvi, wakulima wa mwani, viongozi wa serikali za mitaa pamoja na viongozi wa Kamati za Uhifadhi (VLCs). Kupitia warsha hiyo, washiriki wamepatiwa elimu kuhusu umuhimu wa maeneo ya bahari yaliyohifadhiwa na nafasi yake katika kulinda bioanuwai, kuimarisha uzalishaji wa samaki na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa jamii za pwani.

 

Mada zilizowasilishwa zimejikita katika umuhimu wa makazi muhimu ya viumbe baharini, yakiwemo miamba ya matumbawe, misitu ya mikoko, nyasi bahari na maeneo ya mito kukutana na bahari, pamoja na mchango wake katika kulinda bioanuwai, kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali za bahari. Uhusiano wa uhifadhi na DIRA ya maendeleo ya Taifa 2050. Aidha, washiriki wamejadili changamoto zinazoathiri makazi hayo, zikiwemo uvuvi haramu, ukataji wa mikoko, uchafuzi wa mazingira na taka za plastiki, huku wakihimizwa kushiriki katika juhudi za uhifadhi kupitia usimamizi shirikishi na uzingatiaji wa sheria.

Warsha hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usimamizi Endelevu wa Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe vya Bahari Tanzania (TASFAM), unaolenga kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari na kuongeza ushiriki wa wadau katika uhifadhi wa mifumo ikolojia ya bahari. Kabla ya kufanyika Mafia, warsha kama hiyo ilifanyika Mtwara tarehe 19 November 2026 ikiwakutanisha wadau wa Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma (MBREMP), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uhifadhi shirikishi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari nchini.

slot gacor